
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Sekta ya Afya, Profesa Tumaini Nagu akizungumza na leo, Agosti 18, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduziPRORota Clinical Trial, utafiti wa kitabibu unaolenga kutathmini iwapo matumizi ya probiotics yanaweza kuongeza ufanisi wa chanjo ya rotavirusi.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu wa MUHAS, Profesa Bruno Sunguya akizungumza na leo, Agosti 18, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi PRORota Clinical Trial, utafiti wa kitabibu unaolenga kutathmini iwapo matumizi ya probiotics yanaweza kuongeza ufanisi wa chanjo ya rotavirusi.


………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) pamoja na taasisi washirika kutoka nje ya nchi, kimezindua PRORota Clinical Trial, utafiti wa kitabibu unaolenga kutathmini iwapo matumizi ya probiotics yanaweza kuongeza ufanisi wa chanjo ya rotavirusi, kupunguza magonjwa ya kuhara kwa watoto na kuchangia katika kukabiliana na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antibiotiki.
Akizungumza leo, Agosti 18, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Sekta ya Afya, Profesa Tumaini Nagu, amesisitiza umuhimu wa utafiti katika kusaidia Serikali kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi, kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuwekeza katika afua zenye manufaa makubwa kwa jamii.
Profesa Nagu amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuimarisha utafiti na ubunifu, programu za chanjo pamoja na mikakati ya kukabiliana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa, huku ikiendelea kuboresha afya ya mama na mtoto kama sehemu ya juhudi za kufikia Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Coverage).
Aidha, amewataka watafiti kutekeleza utafiti huo kwa kuzingatia viwango vya juu vya uadilifu wa kisayansi, maadili ya utafiti na ushirikishwaji wa jamii.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuhakikisha matokeo ya utafiti yanatafsiriwa kuwa sera na vitendo vinavyoweza kuboresha afya ya watoto.
“Utafiti huu unaonesha umuhimu wa kujenga ushirikiano wa muda mrefu kati ya taasisi za ndani na kimataifa katika kuzalisha maarifa, kujenga uwezo wa wataalamu na kuhakikisha ushahidi wa utafiti unawafikia watunga sera na watoa huduma za afya,” amesema Profesa Nagu.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu wa MUHAS, Profesa Bruno Sunguya, amesema PRORota ni mfano wa umuhimu wa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto changamano za afya.
Amesema hakuna taasisi moja inayoweza kukabiliana kwa ufanisi na changamoto zote za afya ya jamii bila kushirikiana na wadau wengine, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha utaalamu, rasilimali na uzoefu kutoka vyuo vikuu, taasisi za utafiti, Serikali, wataalamu wa afya na washirika wa kimataifa.
Utafiti huo unawakutanisha wataalamu kutoka nyanja mbalimbali, zikiwemo microbiology, infectious diseases, epidemiology, health economics, social sciences na public health.
“Ushirikiano huu unahusisha
watafiti na taasisi kutoka Tanzania, Norway, Malawi na Côte d’Ivoire, na unaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuzalisha ushahidi,” amesema Profesa Sunguya.
Profesa Sunguya amesema PRORota inaendana na dhamira ya MUHAS ya kuimarisha utafiti, ubunifu na uzalishaji wa ushahidi wa kisayansi unaoweza kutumika kuboresha afya ya wananchi na kusaidia Serikali katika kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi.
Ameeleza kuwa, kwa kuungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na washirika wa maendeleo, MUHAS imeendelea kukuza mazingira bora ya ufundishaji na utafiti, kuimarisha uwezo wa watafiti na kujenga ushirikiano wa kitaifa na kimataifa katika maeneo mbalimbali ya afya.
PRORota inalenga kushughulikia changamoto za magonjwa ya kuhara kwa watoto na usugu wa vimelea dhidi ya dawa. Magonjwa ya kuhara yanaendelea kuwa miongoni mwa sababu muhimu za maradhi na vifo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Utafiti huo unalenga kutathmini iwapo probiotics zinaweza kutumika kama nyongeza katika kuboresha ufanisi wa chanjo ya rotavirus na hivyo kusaidia kupunguza magonjwa ya kuhara kwa watoto.
Aidha, utafiti unalenga kuchunguza iwapo hatua hiyo inaweza kuchangia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya antibiotiki na hatimaye kusaidia katika kukabiliana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa (antimicrobial resistance – AMR).
Matokeo ya utafiti yanatarajiwa kutoa ushahidi wa kisayansi ambao unaweza kusaidia katika kuandaa na kuboresha sera, miongozo na mifumo ya utoaji wa huduma za afya, hususan katika maeneo ya afya ya mtoto, chanjo na matumizi sahihi ya antibiotiki
