NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA 

SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hassan Kabeke, amesema Halmashauri ya BAKWATA mkoani hapa iliyomaliza muda wake haikulala usingizi katika suala la maendeleo, imetekeleza miradi ya maendeleo ikitumia zaidi ya sh. milioni 203. 

Akizungumza leo, baada ya uchaguzi wa viongozi wa Halmashauri ya BAKWATA Mkoa wa Mwanza, Sheikh Kabeke alisema fedha hizo sh. milioni 203 zimetumika katika ujenzi wa ofisi ya baraza hilo mkoa, huku  kitega uchumi kilichosimama kwa takribani miaka 15 kikiendelea. 

Alisema pia ujenzi wa vituo vya afya umeendelea, ambapo kituo cha Ilemela kimekamilika, huku Sengerema jengo la wagonjwa wa nje (OPD) likikamilika. 

Sheikh Kabeke alisema katika Wilaya ya Kwimba, BAKWATA imenunua kiwanja chenye ukubwa wa ekari tano, huku misikiti ikijengwa katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Lunele, Chambwa na Mwabomba, pamoja na kufanyika kwa maboresho ya Msikiti wa Mantare.

Alisema pia viwanja na nyumba za wakfu zimekabidhiwa BAKWATA, akisema hatua hiyo imewezekana baada ya Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zuber Mbwana Bin Ally kurejesha imani kwa Waislamu na hivyo kuimarisha usimamizi wa mali za wakfu ambazo, kwa kipindi cha nyuma, hazikuwa zikifanyika kwa kiwango kinachotarajiwa.

Aidha, alisema walimu wa madrasa pamoja na makatibu wa wilaya za Sengerema, Ukerewe, Magu, Kwimba na Misungwi wamepatiwa pikipiki kwa ajili ya kurahisisha usafiri na utekelezaji wa majukumu yao.

Sheikh Kabeke aliwataka viongozi na wajumbe wapya wa Halmashauri ya BAKWATA Mkoa wa Mwanza kutoridhika na yaliyofanyika, bali mkayaishi, kuyaendeleza na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ili ifikapo mwaka 2030, baada ya kumalizika kwa kipindi chao cha miaka mitano, wawaeleze Waislamu mambo yaliyotekelezwa.

“Wajumbe hamjapoteza kitu, mmekuja kutengeneza dini yenu.Waislamu wakikosa maendeleo na mradi, ninyi wajumbe mnahusika na mtawajibika.Waislamu sasa hawataki maneno ya ‘tuta’, bali tuna, mafanikio mnayoyaona  haya ni kujitoa na kujitolea, mazuri yalyofanyika tuendee kuyaishi na kuwaombea wazee badala ya kuwabeza kuwa hawakunya kitu, ” alisema.

Akizungumzia wagombea ambao hawakupata kura za kutosha katika uchaguzi huo, Sheikh Kabeke alisema hawapaswi kutengwa kwa sababu nia yao ya kugombea ilikuwa ni kusaidia kuleta maendeleo ya Waislamu. “Mliogombea, kura hazikutosha, nia yenu ilikuwa kuleta maendeleo, hatuwezi kuwaacha. Bado mnayo nafasi ya kufanya ndani ya baraza lenu, kazi zipo za kutosha,” alisema.

Katika uchaguzi huo, Bakari Twaha Utalii alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza baada ya kupata kura 38 kati ya kura 40 zilizopigwa, Rajabu Hamis Rajabu  alitangazwa kuwa Mjumbe wa Taifa baada ya kupata kura 38 kati ya kura 40 halali.

Kwa upande wa Baraza la Masheikh, wajumbe tisa walichaguliwa kati ya wagombea 12 nao ni Adam Ramadhan Ndaki , Hussein Jumanne Saad  na Mansour Ramadhan Msunu waliopata kura 39  kila mmoja, Amri Zuberi Luhende kura 38, Mohamed Baruti Zeyd na Saad Omari Suleman kura 37 , Rashid Abdallah Ferej , Simba Ramadhan Simba na Yasin Ramadhan Msunu kura 35 kila mmoja. 

Wajumbe 10 wa Halmashauri ya Mkoa waliochaguliwa ni Abdi Mussa Hanzuruni na  Bakaran Omar Ramadhan, Mussa Issa Baruan na Mohamed Said Mohame kura 37 kila mmoja,  Idrisa Haesh na Mansour Marzuku Magongo kura 36 kila mmoja, Hamis Suleiman Gariyatano na  Yahya Nassar Hussein kura 34 kila mmoja, Nassoro Makonge Issa kura 32 na Yasir Said Fuad kura 29. 

Akizungumza baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo, Msimamizi wa uchaguzi, Mohamed Khamis Said, aliwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa ushirikiano wao uliowezesha mchakato huo kukamilika kwa utulivu na weledi.

“Niwashukuru kwa dhati ya moyo wangu wajumbe wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi huu kwa mapokezi na ushiriki wenu uliowezesha mchakato wa uchaguzi kukamilika. Bila ushirikiano wenu uchaguzi ungekuwa mgumu; si rahisi kufanya chaguzi mbili kwa weledi na utulivu mkubwa,” alisema.

Aliwakumbusha viongozi waliochaguliwa kuwa wana jukumu la kulipeleka mbele Baraza la BAKWATA Mkoa wa Mwanza kwa kuendeleza maendeleo na kusimamia majukumu waliyopewa.