Na: OWM – TAMISEMI, Dodoma
Mkutano Mkuu wa 16 wa Mwaka wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA) unatarajiwa kujadili mchango wa ugatuzi wa madaraka katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku ukilenga kuweka mikakati itakayowezesha wananchi kunufaika zaidi na usimamizi wa maendeleo katika maeneo yao.
Mkutano huo utafanyika Agosti 19–21, 2026 katika Ukumbi wa Jiji la Dodoma, Mji wa Serikali Mtumba, ukiwa na Kaulimbiu isemayo: “Ugatuzi wa Madaraka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni nguzo madhubuti ya kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa TOA, Bw. Albert Gabriel Msovela, ambaye amesema Mgeni Rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye atauzindua rasmi Agosti 19, 2026.
Bw. Msovela amesema mkutano huo unaendana na maelekezo ya Serikali yanayochagizwa na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wananufaika na ugatuaji wa madaraka, hususan katika usimamizi wa miradi ya maendeleo na upatikanaji wa huduma bora za kijamii, kama zilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Mkutano huu ni fursa kwa wajumbe kujadili maeneo yaliyoainishwa kwenye Dira, na tutakuwa na mada mbalimbali zitakazowasilishwa na wabobezi. Ninawaomba wananchi waufuatilie mkutano huu utakaokuwa mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya habari ili wajue ni kwa namna gani TOA itawashirikisha kwenye ubunifu na usimamizi wa miradi yote, ikiwemo ya afya, elimu na miundombinu ya barabara,” amesema Bw. Msovela.
Aidha, Bw. Msovela amesema mkutano huo unatarajiwa kutoa maazimio na mikakati ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya moja kwa moja kutokana na uwepo wa kikao hicho.
Ametoa wito kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu huo kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika mijadala itakayofanyika, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kujenga mikakati yenye tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Wajumbe watakaoshiriki katika Mkutano Mkuu huo wa TOA ni Makatibu Tawala wa Mikoa yote 26, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, zikiwemo Jiji, Manispaa na Halmashauri, pamoja na Makatibu Tawala wa Wilaya zote 136 nchini.

