Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko, akizungumza wakati wa ziara ya Kamati katika Chuo cha VETA Bahi, Dodoma.
Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeipongeza Serikali kupitia VETA kwa kuendelea kutoa mafunzo yanayoendana na mahitaji ya jamii, huku ikitaka kuongezwa kwa fani za kilimo na ufugaji katika Chuo cha VETA Bahi, mkoani Dodoma.
Hayo yamebainishwa Agosti 15, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Husna Sekiboko, wakati Kamati ilipotembelea Chuo cha VETA Bahi kukagua shughuli za mafunzo na maendeleo ya chuo hicho.
Amebainisha Kuwa fani zinazotolewa chuoni hapo zinaendana na mahitaji ya jamii inayozunguka chuo, akisisitiza kuwa VETA inapaswa kutoa mafunzo yanayozingatia mazingira na shughuli za kiuchumi za maeneo husika.
Amesema kutokana na mazingira ya Bahi, kuna umuhimu wa kuongeza fani za kilimo na ufugaji ili wanafunzi wapate ujuzi wa vitendo unaoweza kusaidia kutatua changamoto na kuongeza fursa za kiuchumi katika jamii.
“Moja tu la kukazania ambalo nilidhani lingeweza kufanyiwa kazi kwa haraka sana ni fani ya kilimo na ufugaji,” amesema Mhe. Sekiboko.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa maji katika chuo hicho utawezesha wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo katika kilimo, bustani na landscaping, sambamba na kuboresha mazingira ya chuo.
Aidha, Mhe. Sekiboko ameitaka Serikali kukamilisha karakana ambazo bado hazijakamilika na kuhakikisha zinapatiwa vifaa vya kisasa vinavyoendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.
Pia ameomba Serikali kutoa ikama ya watumishi wa VETA nchini, ikionyesha idadi ya waliopo, wanaokosekana na kiwango cha upungufu, ili kusaidia kupanga mahitaji ya ajira za wakufunzi.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema ujenzi wa vyuo 25 vya VETA vya wilaya ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuongeza fursa za elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Amebainisha kuwa Chuo cha VETA Bahi kina eneo lenye ukubwa wa ekari 50, hivyo kuna nafasi ya kuongeza majengo na miundombinu kulingana na mahitaji ya chuo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa VETA, Dkt. Abdullah Ngodu, amesema wanafunzi 416,000 wamepata fursa za elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026, wakiwemo wenye mahitaji maalumu 1,830 na wanaotoka katika mazingira magumu 6,515.
Aidha, ameongeza kuwa VETA imetoa mafunzo kwa wajasiriamali 6,501 na wafanyakazi 1,113, huku ikifanya tafiti 13 za soko la ajira na uchambuzi wa mahitaji ya ujuzi ili kuandaa mitaala inayozingatia mahitaji ya kiuchumi ya maeneo husika.

