NA DENIS MLOWE, IRINGA 
UMOJA wa wanawake (UWT) wa CCM Kata ya Mtwivila, Manispaa ya Iringa, wamekabidhiwa mradi wa magogo kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi, kuongeza kipato na kuwaondoa katika utegemezi wa mikopo yenye masharti magumu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mradi huo, Diwani wa Viti Maalum anayewakilisha maeneo ya Gangilonga, Mtwivila na Isakalilo, Sara John Ponela, amesema ameamua kuanzisha mradi huo baada ya kubaini kuwa wanawake wa kata hiyo hawakuwa na mradi wa pamoja wa kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Ponela amesema mradi huo unalenga kuwa chanzo cha mapato kwa wanawake hao na kuwawezesha kuanzisha miradi mingine, huku wakijenga mfuko wa pamoja ambao utawasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za kifamilia na kiuchumi.
Amesema wanawake wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi, ambapo asilimia nne hutengwa kwa wanawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.
“Niliona kama diwani lazima nije na suluhisho kwa sababu wamenichagua na wananitegemea. ndio maana nikaamua kuleta mradi huu ili wanawake waweze kujiendesha kimaisha na kujikwamua kiuchumi,” amesema Ponela.
Ameongeza kuwa mradi huo pia utasaidia kupunguza utegemezi wa mikopo isiyo rasmi yenye riba na masharti magumu, ambayo amesema imekuwa chanzo cha changamoto kwa baadhi ya wanawake.
Ponela alisema kuwa mradi huo umegharimu takribani Sh milioni moja, huku magogo hayo yakitoka New Forest, Wilaya ya Kilolo, na kusisitiza kuwa mradi huo ni wa kikundi na si wa mtu mmoja.
Amesema mfumo wa uendeshaji wa mradi umeandaliwa kwa namna ambayo fedha zitakazopatikana zitawekwa kwenye mfuko wa pamoja na matumizi yatafanyika kwa maamuzi ya kikundi, jambo litakalosaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Ponela amewataka wanawake hao kuutumia vizuri mradi huo na kuahidi kuwa iwapo utaendeshwa kwa ufanisi, utaweza kukua na kuongeza idadi ya magogo yanayosafirishwa na hatimaye kuwa chanzo kikubwa cha kipato kwa wanawake wa Kata ya Mtwivila.
“Ukimwinua mwanamke, umeiinua familia. Leo mmeona lori moja, lakini ninaamini baada ya miezi michache tunaweza kuona malori mengi zaidi kama mradi huu utaendeshwa vizuri,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Kata ya Mtwivila, Amina Karuma, amempongeza Diwani Ponela kwa kuwa na maono ya kuanzisha mradi huo, akisema wanawake wengi katika kata hiyo ni walezi wa familia na wanahitaji fursa za kiuchumi zitakazowawezesha kujitegemea.
Karuma amesema mradi huo umekuwa chachu mpya kwa wanawake wa Mtwivila na kuahidi kuwa uongozi wa UWT utahakikisha unalindwa na kusimamiwa kwa uadilifu ili uweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Naye Mwenyekiti wa mradi huo, Hidaya Mpogole, amesema mradi huo umeleta matumaini mapya kwa wanawake na kwamba wana mpango wa kutumia faida watakazopata kuanzisha biashara nyingine.
Amesema pia wanakusudia kujenga mfuko wa pamoja utakaotumika kuwasaidia wanachama wakati wa changamoto mbalimbali, ikiwemo maradhi, misiba na mahitaji mengine muhimu.
Kwa upande wake, Katibu wa UWT Kata ya Mtwivila, Zuhura Wasi, amewataka wanawake kuutunza na kuusimamia kwa umakini mradi huo ili uweze kukua na kuwa chanzo cha maendeleo kwao.
Wasi amesema wanawake wanapaswa kuachana na mikopo yenye masharti magumu na badala yake kutumia mapato ya mradi kujenga mtaji wa pamoja, kuongeza biashara na hatimaye kuanza kukopeshana wao kwa wao.
Amesema endapo mradi huo utasimamiwa kwa umakini, wanawake wa Kata ya Mtwivila wataweza kujikwamua kiuchumi na kuwa mfano kwa maeneo mengine.