Na; Mwandishi Wetu
Unguja
TIMU ya Kundemba FC imetawazwa mabingwa wapya wa Mashindano ya PBZ Yamle Yamye kwa kuichapa bao 1-0 timu ya Ubinadam Kazi FC lililofungwa na Abdallah IddI Pina katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mashindano hayo yalishirikisha timu 36 kutoka Unguja timu 24 na Pemba timu 12 yakiwa katika msimu wa nane, hivyo kuifanya Kundemba FC kuzawadiwa kitita cha Shilingi 20M huku mshindi wa pili akikabidhiwa kiasi cha Shilingi 10M.
Pamoja na Kundemba FC kuzawadiwa kiasi hicho cha fedha kama bingwa lakini mlezi wa timu hiyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Zanzibar, Mhe. Hamad Yussuf Masauni inapotokea timu hiyo aliwapongeza kwa kuwapa kiasi cha shilingi 10M.
Mhe. Masauni ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) amesema ataendelea kuisapoti timu hiyo ili kuona vijana wananufaika na vipaji vyao kupitia mchezo wa soka.
“Soka ni moja ya ajira ambayo watu wanalipwa fedha nyingi, ndio maana serikali kwa kutambua hilo imeweka mazingira mazuri ili vijana waweze kukuza vipaji vyao kwenye mazingira mazuri na salama.
“Nitasimama pamoja na nyie kuhakikisha Timu ya Kundemba inakuwa kimbilio la wengi kujifunza kwa namna ambavyo mmekuwa wavumilivu katika kutafuta mafanikio ambayo leo hii kila mmoja anafurahia,” amesema Mhe. Masauni.
Akimtolea mfano mchezaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuwa ni moja ya wachezaji wazawa wanaolipwa pesa nyingi kutokana na kipaji chake ambacho siri kubwa ni kujituma na kuwa na nidhamu.
Kwa upande wake, Katibu wa timu hiyo, Masoud Bajuni amemshukuru Mhe, Masauni kwa namna ambavyo amekuwa kimbilio kwa wengi hasa vijana, akisisitiza kuwa uongozi utaendelea kuisimamia timu ili kuleta mafanikio zaidi.
“Leo umetimiza ahadi ambayo uliitoa, na mimi kwa niaba ya wenzangu nikuahidi kuwa tutaisimamia timu kwa nguvu zote ili kuepuka migogoro ambayo inaweza kutuvuruga na mwisho wa siku tukapoteza lengo.”
Naye, nahodha wa timu hiyo, Hassan Banzu ameeleza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya timu na uongozi kwa kushikamana hadi kufika fainali jambo ambalo halikuwa rahisi.

