Na Mwandishi Wetu, Namtumbo
WANANCHI wa kata ya Mputa Halmashauri ya wilaya Namtumbo mkoani Ruvuma, wamepata tumaini jipya la usalama wa afya zao baada ya mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Homera kukabidhi gari jipya la kubeba wagonjwa (Ambulance).
Mganga mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Fatma Gama,kituo hicho kwa sasa kina hudumia wananchi zaidi ya 13,831 wanaoishi katika kata ya Mputa umbali wa kilometa 98 kutoka hospitali ya wilaya Namtumbo.
Dkt. Gama alieleza kuwa, umbali wa kutoka Mputa hadi hospitali ya wilaya iliyopo Namtumbo mjini unaonesha umuhimu mkubwa wa kuwa na gari la wagonjwa kwa ajili ya kuwawezesha wagonjwa wanaohitaji huduma za juu zaidi kufikishwa hospitalini kwa haraka.
Dkt. Gama ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Homera kwa jitihada kubwa za kuhakikisha huduma za afya zinaimarishwa na changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi.
“Leo tunashuhudia matokeo ya jitihada hizo kupitia upatikanaji wa gari hili la wagonjwa(Ambulance) ambalo litakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za dharura za afya hususani kwa mama wajawazito,watoto,wagonjwa mahututi na wananchi wengine wanaohitaji huduma za haraka za matibabu”alisema Dkt Gama.
Alisema kutokana na umbali wa kilometa 98 kutoka kituo cha afya Mputa hadi Hospitali ya wilaya ni ukweli kwamba gari hilo ni msaada mkubwa kwani litasaidia kupunguza ucheleweshaji wa kuwafikisha wagonjwa katka vituo vya huduma za juu pale inapohitajika,hivyo kuokoa maisha na kuboresha matokeo ya huduma za afya.
Aidha alisema,upatikanaji wa gari hilo ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Homera katika kusikiliza,kuwasemea na kutatua changamoto za wananchi sambamba na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya nchini.
Naye mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mputa Dkt Tumaini Kisimbo,ameishukuru serikali kutoa kiasi cha Sh.milioni 500 kwa ajili ya kujenga majengo manne katika kituo cha afya Mputa.
Dkt. Kisimbo ametaja majengo mapya yanayojengwa katika Kituo hicho Kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma za afya ni jengo la wagonjwa wan je(OPD)kwa gharama ya Sh.milioni 195,217,000,jengo la maabara Sh.34,956,000,jenga la mama na mtoto na chumba cha upasuaji Sh.255,299,845.09,jengo la nishati litakalogharimu Sh.9,567,000 na Sh.5,000,000 zitatumika kuunganisha nishati ya umeme.
Alisema utekelezaji wa mradi huo ulianza mwezi julai 2026 na unatarajia kukamilika mwezi oktoba kwa mujibu wa mikataba na mafundi.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Juma Homera alisema,serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi ilizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Dkt. Homera ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria alisema,gari hilo litakuwa Mputa ili kuwahudumia wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda hospitali nyingine kwa ajili ya huduma za uchunguzi zaidi wa afya zao.
“Nimuombe dereva atakayeendesha gari hili awe makini barabarani,siku za nyuma kuna gari liliharibika kutokana na uzembe wa dereva,kwa hiyo gari hili likianguka na dereva ahakikishe ananguka,hauwezi kuendesha gari la wagonjwa ovyo ovyo,waendeshe wagonjwa vizuri na wafikishe hospitali ya wilaya vizuri,ukiendesha kwa fujo na ukaharibu maana yake umewauwa wananchi wa Mputa na sisi hatutakubali “alisema Dkt Homera.
Kuhusu kituo cha afya Dkt Homera alisema, tayari serikali imetoa Sh.milioni 500 kwa ajili ya kujenga jengo la wagonjwa wa nje na majengo mengine ikiwemo jengo la upasuaji ili akina mama wanaohitaji huduma ya upasuaji waweze kupata huduma hiyo karibu na maeneo yao.
“Wananchi wenzangu wa Mputa tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwa moyo wa upendo,kwani licha ya kutupatia gari la wagonjwa,lakini ametoa fedha Sh.milioni 500 ili kuboresha kituo chetu cha afya,nawaomba tunendelee kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya”alisema Dkt Homera.



