Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wakulima na teknolojia, huduma za kitaalamu, masoko pamoja na fursa za uwekezaji na mikopo, akitaja mambo manne muhimu ambayo wananchi watakapoyatembelea wataweza kuyaona na kujifunza.Akizungumza wakati alipotembelea mabanda mbalimbali ya Wizara ya Kilimo na taasisi zake, Bw. Mweli amesema jambo la kwanza ni uwezo wa Dodoma kuzalisha mazao mbalimbali, akisisitiza kuwa dhana kwamba Dodoma ni jangwa si sahihi, kwani katika eneo la Nanenane pekee kuna mazao yakiwemo pamba, korosho, tumbaku na mazao ya matunda kama tufaa yanayostawi kutokana na matumizi ya teknolojia na mifumo sahihi ya uzalishaji.

Amesema Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kuwekeza kwa nguvu katika miundombinu ya umwagiliaji, huku bajeti ya Tume hiyo ikiwa zaidi ya Shilingi bilioni 300, hatua inayolenga kuwawezesha wakulima kupata maji ya uhakika na kuongeza uzalishaji.

Jambo la pili, amesema ni uwepo wa teknolojia mbalimbali za kilimo, ambapo zaidi ya waoneshaji 200 wanashiriki katika kuonesha teknolojia na ubunifu unaoweza kutumiwa na wakulima kuongeza tija. Amesema mwaka huu Serikali itaendelea kugawa mashine 100 za kubangua korosho kupitia Bodi ya Korosho, ambapo kila mashine ina uwezo wa kubangua zaidi ya tani 80 kwa siku na zitakabidhiwa kwa vikundi vya wakulima.

“Kila mwaka tutatoa mashine 100,” amesema Bw. Mweli, akieleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha wakulima wadogo, wanawake na vijana kutumia teknolojia kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao yao.

Jambo la tatu, amesema ni muunganiko uliopo kati ya watoa huduma mbalimbali na wakulima, ambapo Nanenane inatoa fursa kwa wananchi kukutana moja kwa moja na wataalamu, taasisi na wadau wanaotoa huduma zinazohusiana na kilimo.

Amesema wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kupata elimu na huduma za kitaalamu, kujifunza teknolojia mpya na kupata majibu ya changamoto zinazowakabili katika shughuli zao za kilimo.

Jambo la nne, amesema ni fursa za upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu, akieleza kuwa zaidi ya taasisi 40 zinazotoa huduma za kifedha na mikopo zinashiriki katika maonesho hayo, hivyo wananchi wanapaswa kufika kujifunza namna ya kupata mitaji kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza shughuli zao za kilimo.

“Natoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki Maonesho haya ya Nanenane ili waweze kujifunza teknolojia, kupata huduma za kitaalamu na kufahamu fursa mbalimbali zinazopatikana,” amesema.

Aidha, Bw. Mweli amesema maonesho hayo yanaendelea kuonesha utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa ghala la chakula la Afrika na dunia, kupitia kuongeza uzalishaji, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo.

Amesema Afrika imeanza kuitambua Tanzania kama nchi yenye uwezo mkubwa wa uzalishaji wa chakula, hivyo maonesho ya Nanenane yanaendelea kujenga nafasi ya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula na ushirikiano wa kilimo barani Afrika.

Kwa upande mwingine, Bw. Mweli amesema Nanenane mwaka huu imeendelea kuvutia washiriki wengi, ambapo waoneshaji 1,188 kutoka ndani ya nchi na waoneshaji 24 kutoka nje ya Tanzania wanashiriki, huku maonesho hayo pia yakipokea wageni mbalimbali wa kimataifa, akiwemo Waziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Sudan Kusini.

Katibu Mkuu ametembelea mabanda ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA), Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani (NAESA), Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Bodi ya Pamba, Bodi ya Sukari, Bodi ya Kahawa, Bodi ya Korosho, Bodi ya Mkonge, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) pamoja na banda la Wizara ya Kilimo.