Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limesema kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kupitia usindikaji kunaweza kupunguza upotevu unaofikia asilimia 40, hususan kwa matunda na mboga ambazo huharibika kwa haraka baada ya kuvunwa.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea viwanja vya John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Mhandisi na Mtafiti wa Teknolojia za Nishati kutoka TIRDO, Mhandisi Augustino Masse, amesema tafiti zinaonyesha kuwa sehemu kubwa ya mazao yanayoharibika inaweza kuokolewa kwa kutumia teknolojia za ukaushaji na usindikaji.
Amesema TIRDO imejikita kuwasaidia wakulima na wajasiriamali kuongeza thamani ya mazao yao ili yafike sokoni yakiwa bidhaa kamili zenye ubora unaokubalika.
“Historia na tafiti zetu zinaonyesha kuwa bidhaa zinazoharibika kwa haraka, hususan matunda na mboga, hupotea kwa kiwango kinachofikia asilimia 40. Sisi TIRDO tumelitambua hilo kama fursa ya kuongeza tija kwa kupunguza upotevu kupitia teknolojia za usindikaji,” amesema Mhandisi Masse.
Amefafanua kuwa kukausha mazao pekee hakutoshi kuyafanya kuwa bidhaa inayoweza kushindana sokoni, bali kuna umuhimu wa kuyaongezea thamani kwa kuyawekea vifungashio bora, nembo za ubora na kupata ithibati ya usalama wa chakula.
“Ukimenya maembe na kuyakausha bado hujakamilisha hatua ya kutengeneza bidhaa. Bidhaa lazima iwe na kifungashio kinachokidhi viwango, nembo ya ubora na ithibati ya usalama wa chakula. Hapo ndipo sisi TIRDO tunawasaidia wajasiriamali ili bidhaa zao zipate vibali kwa urahisi na kuingia sokoni,” amesema.
Aidha, amesema taasisi hiyo pia hutoa huduma za ukaguzi wa mifumo ya uzalishaji kwa lengo la kupunguza gharama za kuongeza thamani wa mazao na hivyo kuongeza kipato cha wakulima na wajasiriamali.
Ameeleza kuwa mabaki ya mazao kama mabua na magunzi ya mahindi yanaweza kutumika kwa njia nyingine za uzalishaji badala ya kuwa taka, jambo linalosaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza ufanisi.
Mhandisi Masse amesema bado Watanzania wamezoea kutumia mazao mabichi pekee, hali inayochangia upotevu mkubwa wa mazao wakati wa msimu wa mavuno.
“Tumezoea kula kila kitu kikiwa kibichi. Ukitaka nyanya unaenda sokoni kununua nyanya mbichi, ukitaka embe unanunua embe bichi. Lakini kiwango kikubwa cha matunda kinachooza wakati wa msimu tunakiona ni jambo la kawaida, kumbe ni hasara kubwa kwa uchumi. Kama tungezuia mazao hayo yasiharibike kwa kuyasindika, tungeongeza akiba ya chakula na hata kuuza ziada kwenye masoko ya nje,” amesema.
Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia za kuongeza thamani wa mazao ni miongoni mwa njia muhimu za kupunguza upotevu wa mazao, kuongeza kipato cha wakulima na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo na viwanda nchini.
