Na Adelina Johnbosco – MAELEZO

Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kimetajwa kuwa kinara katika mafunzo ya anga ndani na nje ya Tanzania katika utoaji wa mafunzo kwa wanafunzi kutoka ndani na nje nchi.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Prosper Mgaya, wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma, katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Mtumba, Agosti 3, 2026, alipokuwa akieleza kuhusu utekelezaji wa Mwaka wa Fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27 wa chuo hicho.

Dkt. Mgaya amesema, mafunzo ya urubani hapa nchini kwa sasa yanafanyika kuanzia ngazi ya mwanzo hadi ya mwisho wanafunzi wanahitimu bila kutegemea msaada wowote kutoka nje. Hii inatajwa kwamba ni kutokana na wataalamu na vifaa vya kutosha walivyonavyo chuoni hapo hali inayofanya mataifa ya nje kuja kupata msaada katika chuo hicho.

“Mashirika ya ndege Kenya na Uganda wameshatutembelea kuangalia ni jinsi gani wataleta wafanyakazi wao kuja kufanya mazoezi kwetu pamoja na kupata uzoefu, pia wahudumu wa Shirika la Ndege Tanzania nao watakuwa wanakuja kuongeza ujuzi chuoni kabla ya kuuhisha leseni zao kila mwaka” amesema Dkt. Mgaya  

Vile vile, amebainisha kwamba, kwa sasa wamedaili wanafunzi 22 wa urubani ambao kati ya hao 18 wamefikia hatua ya kurusha ndege wenyewe huku 4 wakiwa tayari wamehitimu na kupata leseni ya awali.

“Kwa hatua hii tuliyofikia, upungufu wa marubani nchini kwetu utapungua kwa kiwango kikubwa hadi kuisha kabisa, lakini hii pia inawapa fursa vijana wetu kupata kazi ndani na katika mataifa ya nje, wengi wameshaajiriwa na shirika letu la ndege, wapo waliomaliza katika sekta ya anga chuoni kwetu na kwa sasa wanafanya kazi Shirika la Ndege la Dubai” Dkt. Mgaya

Akieleza kuhusu mkakati wa Serikali kuikuza sekta ya utaalam wa anga nchini, Dkt. Mgaya amesema, kwa sasa wamepewa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili ya urushaji wa ndege kwa vitendo, ila kwa kuwa kina shughuli nyingi, tayari Serikali imewapa eneo jipya katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kufanya mazoezi.

“Eneo hilo lina heka 60 na Shilingi bil 5.83 zimetolewa kujenga miundombinu kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kurusha ndege, ujenzi umefika asilimia 80 na tunategemea kabla ya Oktoba 2026 tutakuwa tumekamilisha, ni sehemu nzuri ya kurukia kwani kuna viwanja vya ndege viwili karibu ambavyo ni Arusha na Moshi vitakuwa vinasaidia katika kuruka na kutua” amefafanua Dkt. Mgaya

Pia, Dkt. Mgaya amesema, mradi huo unahusisha ujenzi wa madarasa ya mafunzo kwa marubani pamoja na karakana ya matengenezo ya ndege, mafunzo ya vitendo kwa wahandisi wa matengenezo ya ndege na huduma za matengenezo ya ndege za mafunzo za chuo.

Kwa mujibu wa taarifa yake, Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bil 12 kwa ajili ya mafunzo ya wahudumu wa ndege, hii inajumuisha kununua vifaa maalum vya kujifunzia na wanafunzi wote wanaomaliza mafunzo mbalimbali katika chuo hicho wanakuwa tayari wanaingia au kukubalika katika soko la ajira popote duniani kwani wanajifunza katika mitaala ya kimataifa.

“Kwa mafunzo ya usafiri wa anga, chuo chetu NIT ni pekee kwa Afrika Mashariki na cha pili Afrika kwa kuwa na vifaa vya kitaalamu vinavyokidhi mahitaji na vya kutosha kikitanguliwa na chuo cha nchini Ethiopia” ameeleza Dkt. Mgaya