Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwakabidhi viongozi, Nyenzo za Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 baada ya uzinduzi, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Agosti, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwakabidhi mfano wa Ufunguo kama ishara ya mtazamo mpya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malick Akil, Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalula pamoja na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara Zanzibar (ZNCC), Bw. Ali Amour baada ya uzinduzi Nyenzo za Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Agosti, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima kutoka Rais wa Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC), Bw. Vicent Minja katika hafla ya uzinduzi wa Nyenzo za Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Agosti, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Nyenzo za Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Agosti, 2026.

Viongozi mbalimbali, wadau wa Sekta Binafsi pamoja na Sekta ya Umma wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Nyenzo za Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Agosti, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi mbalimbali kabla ya kuzindua Nyenzo za Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Agosti, 2026.
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitaka Taasisi za sekta binafsi kuchukua nafasi kubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuongeza uwekezaji, uzalishaji, matumizi ya teknolojia na ubunifu, huku ikiahidi kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Akizungumza leo Ikulu, Jijini Dar es Salaam, wakati wa Mkutano Maalum wa Serikali na Sekta Binafsi kuhusu Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Rais Dkt. Samia , amesema mafanikio ya dira hiyo yanategemea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi.
Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa amani na utulivu ni nguzo muhimu ya maendeleo, akieleza kuwa mazingira salama ndiyo yanayowapa wawekezaji imani ya kuwekeza, wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa uhakika na wananchi kupata ajira.
Amehimiza uwekezaji unaojumuisha wazalishaji wakubwa na wadogo, matumizi ya wazabuni wa ndani pamoja na kuwashirikisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika shughuli za uzalishaji na mnyororo wa thamani.
Aidha, Rais amewataka wafanyabiashara kuongeza thamani ya rasilimali za ndani, kuzingatia viwango vya ubora na kupanua biashara katika masoko ya Afrika Mashariki, SADC, Afrika na dunia ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.
Pia ameigiza Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuhakikisha wadau wote wanapatiwa elimu kuhusu nyenzo hizo ili kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dira hiyo.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa Dira 2050, akitaja sayansi, teknolojia, uchumi wa kidijitali, uchumi wa buluu, uwekezaji na maendeleo ya rasilimali watu kuwa maeneo ya kipaumbele.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema maboresho ya sera na mazingira ya biashara yameongeza imani ya wawekezaji, huku uwekezaji katika kampuni changa za teknolojia ukiendelea kukua katika sekta za fedha, kilimo na nishati safi.
Kwa niaba ya sekta binafsi, Rais wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula, amepongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha sera, sheria na mifumo ya uwekezaji, akiahidi kuwa sekta binafsi itaendelea kushirikiana na Serikali kuongeza uwekezaji, teknolojia na fursa za ajira.
Katika mkutano huo Rais Samia amezindua nyenzo za utekelezaji wa Dira 2050 na kukabidhi Ufunguo wa Mtazamo Mpya, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa uwazi na uaminifu kati ya Serikali na sekta binafsi.
Pia wamesaini Tamko la Pamoja kati ya Serikali na Sekta Binafsi kuhusu utekelezaji wa Dira 2050.
Katika hatua nyengine Rais Samia ametunukiwa Tuzo ya Heshima kutoka Sekta Binafsi Tanzania kwa kutambua mchango wake katika kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji na kukuza uchumi jumuishi nchini.
