Wananchi mbalimbali wametembelea katika banda la Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) inauoshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, kwa kuonesha teknolojia na ubunifu mbalimbali unaolenga kuongeza thamani ya mazao, kuhamasisha maendeleo ya viwanda na kukuza uchumi wa wananchi.
Kupitia banda lake, TIRDO inatoa elimu kwa wakulima, wajasiriamali na wawekezaji kuhusu teknolojia mbalimbali zinazorahisisha uzalishaji, uchakataji wa mazao na utengenezaji wa bidhaa zenye ubora zinazoweza kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi. Wageni wanaotembelea banda hilo pia wanapata fursa ya kujifunza kuhusu huduma za utafiti, ubunifu na ushauri wa kitaalamu zinazotolewa na taasisi hiyo.
TIRDO imewahimiza wananchi kutembelea banda lake wakati wa maonesho hayo ili kujionea teknolojia zilizobuniwa na wataalamu wa Kitanzania pamoja na kupata elimu itakayowasaidia kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji na kuchangia maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.



