Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya utafiti wa kilimo ili kuhakikisha teknolojia na ubunifu unaozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) unawanufaisha wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.
Akizungumza August 2,2026 jijini Dodoma baada ya kushiriki Marathon ya kuadhimisha miaka 10 ya TARI, Mhe. Chongolo amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana na taasisi hiyo katika kipindi cha muongo mmoja yamechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Aidha, amebainisha kuwa tafiti zinazofanywa na TARI zimewezesha kupatikana kwa teknolojia na mbegu bora zinazowasaidia wakulima kuzalisha kwa ufanisi zaidi, huku zikiwapa uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.
Pia ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika tafiti na kuimarisha ushirikiano kati ya TARI, taasisi nyingine za utafiti na wadau wa maendeleo ili matokeo ya tafiti yaweze kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini.
Marathon hiyo, iliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, iliwakutanisha viongozi wa Serikali, watafiti, wadau wa sekta ya kilimo na wananchi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya TARI yanayoambatana na maonesho ya teknolojia za kilimo, utoaji wa elimu na huduma za ushauri wa kitaalamu.
