Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameielekeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuongeza uwezo wake wa kifedha na kupanua wigo wa utoaji wa mikopo ili kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi nchini, akisema hatua hiyo itachochea mageuzi ya sekta ya kilimo na kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma, amesema kuwa Serikali inaiona TADB kuwa chombo muhimu cha kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wazalishaji na wawekezaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha uwezo wa benki hiyo ili ikidhi mahitaji yanayoongezeka.
Amebainisha kuwa Serikali haiwezi kutegemea ruzuku pekee kila mwaka katika kuendeleza sekta ya kilimo, bali inahitaji taasisi imara ya kifedha itakayowawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata mikopo kwa wakati, kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Aidha, amesema kuwa TADB inapaswa kuongeza ufadhili wa ununuzi wa mbolea, pembejeo, zana za kisasa za kilimo pamoja na miradi ya kuongeza thamani ya mazao, akieleza kuwa hatua hiyo itaongeza tija, ushindani wa bidhaa za Tanzania na kipato cha wazalishaji.
Pia ameelekeza benki hiyo kushirikiana kwa karibu na Wizara za Kilimo na Mifugo pamoja na TAMISEMI kuwekeza katika miundombinu ya baada ya mavuno, hususan ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao ili kuimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa kutumia mazao yao kama dhamana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema kuwa benki hiyo imeendelea kutekeleza jukumu lake la kufadhili miradi ya kimkakati inayochochea maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 700 zimetolewa kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji nchini.
Ameongeza kuwa mafanikio ya uzalishaji wa kahawa kupitia vyama vya ushirika vya mikoa ya Kagera na Kigoma ni miongoni mwa vivutio vikubwa katika banda la TADB, jambo linaloonesha mchango wa benki hiyo katika kuongeza thamani ya mazao na kuwawezesha wakulima.
Aidha, amebainisha kuwa TADB pia imewezesha mradi wa kisasa wa ufugaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo unaotumia teknolojia kutoka Misri wenye uwezo wa kuhifadhi hadi tani 90 za samaki kwa mwezi. Amesema kuwa uwekezaji huo umechangia kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni, kuongeza ajira kwa Watanzania na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo na uvuvi katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

