Mhasibu Mkuu Msaidizi wa Serekali – Usimamizi wa Mifumo na Viwango vya Hesabu kutoka Wizara ya Fedha, Bi. Veronica Kishala amefunga mafunzo ya siku sita kwa Waambata Fedha na watumishi wa Wizara mbalimbali, Julai 25 2026 katika Ofisi za Mahakama, mkoani Morogoro.
Mafunzo hayo yalihusu uandaaji wa Taarifa za Uendelevu (ESG/Sustainability Reporting) na Mfumo wa Usimamizi wa Mali za Serikali (GAMIS).
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Bi. Kishala aliwapongeza washiriki kwa kukamilisha mafunzo yaliyolenga kuwaongezea ujuzi wa kitaalamu katika uandaaji wa taarifa za uendelevu kwa kuzingatia viwango vinavyotambulika kimataifa vya IFRS S1 na IFRS S2, pamoja na matumizi ya Mfumo wa Serikali wa Usimamizi wa Mali (GAMIS). Alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha uwajibikaji, uwazi na ujumuishaji wa masuala ya maendeleo endelevu katika shughuli zote za Serikali.
Alibainisha kuwa maarifa yaliyopatikana yatawawezesha Waambata Fedha kuboresha ubora wa taarifa za kifedha na za uendelevu, kuimarisha usimamizi wa mali za umma na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao, sambamba na kufanikisha malengo ya Serikali ya maendeleo endelevu.
Kwa upande wao, Waambata Fedha walieleza shukrani kwa Wizara ya Fedha na wawezeshaji wa mafunzo hayo, wakisema yameimarisha uwezo wao wa kitaalamu na kuwaongezea uelewa kuhusu mbinu za kisasa za usimamizi wa fedha, uandaaji wa taarifa za uendelevu na matumizi ya mfumo wa GAMIS. Walieleza utayari wao wa kutumia maarifa hayo katika vituo vyao vya kazi ili kuendelea kuboresha utendaji, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma.

