Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Notker Kilewa ameitaka jamii kuwakumbuka watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

Hayo amezungumza Julai 25, 2026 alipowaongoza Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoani humo kutembelea na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha Nuru Orphans Center kilichopo Uyole Jijini Mbeya.

Aidha SSP Kilewa alisema kuwa, Jeshi la Polisi kama sehemu ya jamii limekuwa likifanya kazi zake kwa kushirikiana na jamii ili kuzuia uhalifu na ajali za barabarani, limetembelea kituo hicho na kutoa vitu mbalimbali kama sehemu ya kurejesha kwa jamii na kama sehemu ya kuguswa na watoto yatima.

“Nalaani vitendo vya baadhi ya wazazi kutupa na kutelekeza watoto na kusababisha wengine kupoteza maisha, wengine kuishi katika mazingira magumu na hata kukosa mahitaji muhimu, haki zao za msingi, nitoe wito kwa jamii kutembelea kituo hiki na kutoa msaada wa mahitaji kwa watoto” alisema SSP Kilewa.

Naye, Meneja wa Kituo hicho Bi. Mary Emily amesema kuwa kituo hicho kilianza mwaka 2006 na kinapokea watoto kuanzia umri wa mwaka 0 na kuendelea, kituo kinapata watoto kutoka Ustawi wa Jamii na hadi sasa kituo kina jumla ya watoto 39.

Vilevile, Bi. Mary amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kuwafikiria na kutoa msaada wa vitu mbalimbali ambavyo vimegusa mahitaji yao. Pia Bi. Mary ametoa wito kwa jamii kuendelea kuwakumbuka watoto wanaoishi katika mazingira magumu na yatima.

Kwa upande wake, mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho tangu mwaka 2006 Melania Nuru amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada na ameiomba jamii kuwasaidia watoto wenye mahitaji. Kwa sasa amemaliza kidato cha nne na anatarajia kuendelea na masomo ya elimu ya juu, hivyo anaiomba jamii kumsaidia mahitaji yatakayomsaidia kukidhi masomo yake.