MABALANGA, KILINDI

 21Julai, 2026

Mbunge wa Jimbo la Kilindi, Mhe. Salehe Mbwana Mhando,ameendelea na ziara yake ya Kuwashukuru Wananchi katika Kata ya Mabalanga, ambapo alikutana na kuzungumza moja kwa moja na wananchi wa vijiji vya Kwengaje na Michungwani na Mabalanga , akimshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na wananchi kwa kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Akizungumza katika mikutano hiyo, Mhe. Mhando alisema wananchi wa Kilindi waliandika historia kwa kumpa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ushindi wa takribani asilimia 98 ya kura, huku yeye akichaguliwa kwa takribani asilimia 97 ya kura za ubunge na Madiwani wote wa kata 21 kutoka chama cha Mapinduzi CCM.

Alisema ushindi huo ni deni la kuwahudumia wananchi kwa vitendo na kuhakikisha ahadi zote za maendeleo zinatekelezwa.

 Mhe. Mbunge alieleza kuwa ndani ya muda mfupi baada ya uchaguzi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa shilingi milioni 78 kupitia Mfuko wa Jimbo, fedha ambazo zimeanza kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo katika Kijiji cha Michungwani.

Kuhusu sekta ya elimu, Mhe. Mhando*l alisema ametembelea shule za Michungwani na Kwengaje, na kusisitiza kuwa ifikapo mwezi Desemba 2026, shule hizo zinapaswa kuwa zimekamilika na kusajiliwa ili zianze kutoa huduma rasmi kwa wanafunzi.

 Ili kuunga mkono juhudi hizo, aliahidi kuchangia mifuko 100 ya saruji kwa shule ya Michungwani pamoja na bati 100 za rangi ya kijani kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa shule Kwengaje.

“Uchaguzi umekwisha, sasa ni muda wa kufanya kazi. Tuungane kuhakikisha shule hizi zinakamilika na zinasajiliwa ifikapo mwezi wa Desemba,” alisema Mhe. Mhando.

Katika sekta ya umeme, Mbunge huyo alieleza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 72 vya Wilaya ya Kilindi, ambapo maeneo ya Mkuyu, Finyiliza na Ndukai yaliyopo katika Kata ya Mabalanga yatanufaika na huduma hiyo.

Akizungumzia migogoro kati ya wakulima na wafugaji, Mhe. Mhando alisema ni lazima matumizi ya ardhi yapangwe kwa ufanisi ili kulinda amani na maendeleo ya wananchi.

 Alikemea vitendo vya baadhi ya watu wanaouza ardhi kiholela, jambo linalochochea migogoro na kuharibu mazingira.

Alisisitiza kuwa wafugaji wengi ni waadilifu, lakini wachache wenye tabia ya kulisha mifugo kwenye mashamba ya wananchi kwa makusudi waache mara moja. 

Aidha, Mhe. Mbunge aliahidi kuendelea kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa maji katika Kijiji cha Michungwani, sambamba na kuboresha miundombinu ya barabara kwa kuifungua na kuiboresha barabara inayounganisha Michungwani na Kwengaje ili iweze kupitika kwa urahisi katika misimu yote ya mwaka.

Ziara hiyo imeendelea kuonyesha dhamira ya Mhe. Salehe Mbwana Mhando ya kusikiliza wananchi, kutatua changamoto zao na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.