Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo akiongea na viongozi wa vitongoji, vijiji, na Kata zilizopo katika mwambao wa ziwa Tanzganyika (hawapo pichani) katika ziara yake ya Siku tatu kuzungukia kata hizo zenye bandari bubu zaidi ya 40 katika Wilaya ya Nkasi.
……………………………………………………………………………………………………………..
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya kitongoji hadi kata kusahau tofauti za kisisasa zilizopo ili kuweza kushirikiana kupambana dhidi ya ugonjwa wa Corona na matokeo yake nguvu zielekezwe katika kuilinda mipaka ya nchi isiingiliwe na watu watakaoweza kuliangamiza taifa kwa kuuleta ugongwa huo.
Mh Wangabo amesema kuwa hadi leo terehe 10.4.2020 mkoa wa Rukwa umewaweka Karantini watu 52 ambapo kati ya hao watu 26 wakiwekwa karantini katika bandari rasmi ya Kirando na kuongeza kuwa katika kata ya Kirando, Kipili pamoja na kata ya Itete kuna bandari bubu 20, wakati kata ya Korongwe na Kabwe zikiwa na bandari bubu 16 ambao viongozi wake alizungumza nao. (9.4.2020)
“Mlinzi wa Kwanza wa nchi ni mwananchi mwenyewe, na mwananchi wa kwanza ni yule ambae yupo kwenye serikali zenu za vijiji na vitongoji, hawa ndio wa kulinda nchi, kwahiyo tusiwakubali hawa watu wanaotaka kupita kwenye njia za vichochoro, njia zisizo rasmi, bandari bubu. Mpo hapa wenyeviti wa vitongoji, wenyeviti wa serikali za vijiji vinavyohusika na bandari bubu, maafisa watendaji wa vijiji hivyo mko hapa, maafisa watendaji wa kata zinazohusika mko hapa, maafisa tarafa na madiwani husika mko hapa, wote muungane bila kujali itikadi za kisiasa, tuungane kulinda nchi yetu, hilo ndio jambo la kwanza,” Alisisitiza.
Mh. Wangabo aliyasema hayo katika kikao kifupi na wenyeviti wa vitongoji na vijiji vyenye bandari bubu pamoja na watendaji wao huku wakiambatana na watendaji wa kata zinazohusika za Kirando, Kipili na Itete pamoja na madiwani wao kilichofanyika katika shule ya Sekondari Kirando ili kuwapa maelekezo ya serikali pamoja na kupewa elimu juu ya ugonjwa wa Corona.
Baadhi ya wenyeviti wa vitongoji na vijiji katika kikao hicho waliweza kufikisha maoni yao juu ya uimarishwaji wa huduma za jeshi la uhamiaji katika vijiji vyao vinavyopokea wageni kutoka katika nchi za jirani ambapo Kamanda wa Jeshi la Uhamiaji mkoa wa Rukwa kamishna Msaidizi Elizeus Mushongi aliwahakikishia kuwa waliyoyawasilisha watayashughulikia ikiwemo suala la walowezi pamoja na wanaoingia nchini kwa njia za panya bila ya vibali rasmi.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kamanga, alisema kuwa zoezi la kuwazuia wageni linakwamishwa na walowezi kutoka nchi hizo za jirani na hivyo kuomba msaada kwa jeshi la uhamiaji kuona namna ya kuwashughulikia walowezi hao ili wasiweze kuwaingiza ndugu zao kutoka katika nchi hizo na hatimae waweze kujilinda na maradhi hatari ya Corona.
Aidha, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisambara Galus Kifunda aliliomba jeshi la uhamiaji kuchukua hatua za haraka kufika katika eneo la tukio mara tu wapatapo taarifa za kuingia kwa wageni hao bila ya vipali katika njia hizo za panya kwani wananchi hawataweza kuwashikilia wageni hao kwa muda mrefu kutokana na hofu ya ugonjwa wa Corona.
Wakiongea kwa nyakati tofauti madiwani wa kata hizo za mwambao wa ziwa Tanganyika waliahidi kutoa ushirikiano kwa serikali katika kupambana na janga la ugonjwa wa Corona na kuongeza kuwa wakati huu sio wa kupuuzia maelekezo na maagizo yoyote ya serikali na hivyo kuahidi kushikamana na kushirikiana kufikisha elimu ya ugonjwa wa Corona katika maeneo yao ya kiutawala.
Diwani wa Kata ya Kipili Mh. Wilbroad Chasukila alisema, “Nina usemi mmoja nilikuwa nikiutumia sana shuleni, kwamba ukiwa na wakati, tenda la wakati, utakuwaja wakati utaukosa wakati, utautafuta wakati hutaupata tena, suala hili la ugonjwa wa Corona ni janga la kitaifa na dunia kwa ujumla, itatugarimu kama hatutatenda la wakati, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa maagizo uliyoyatoa tutayafanyia kazi na tutayatendea haki”.