Happy Lazaro, Arusha.

Arusha.Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, amewataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara akisema hatua hiyo ni muhimu katika kugundua magonjwa mapema na kuongeza nafasi ya kupata matibabu kwa wakati.

Makonda ameyasema hayo leo jijini Arusha alipofanya ziara katika kambi ya matibabu ya bure inayoendelea kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, ambapo mamia ya wananchi wanaendelea kunufaika na huduma mbalimbali za uchunguzi na matibabu zinazotolewa na wataalamu wa afya.

Amesema huduma hizo hazilengi tu kutibu wagonjwa, bali pia kutoa elimu ya afya kwa jamii ili wananchi waelewe umuhimu wa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara na kuchukua hatua mapema wanapobaini changamoto za kiafya.

Kwa mujibu wa Makonda, wananchi wengi hupoteza maisha kutokana na kuchelewa kubaini magonjwa, hali ambayo inaweza kuepukika endapo watakuwa na utamaduni wa kufanya vipimo vya afya hata wanapojisikia kuwa wazima.

Amewasisitiza wananchi kufuata maelekezo yote watakayopatiwa na madaktari, kutumia dawa kwa usahihi, kuhudhuria kliniki za ufuatiliaji wanazoelekezwa na kutunza vifaa vya tiba wanavyopewa ili viendelee kuwasaidia baada ya kuondoka kambini.

Makonda amebainisha kuwa kufanikisha kambi hiyo kumetokana na ushirikiano wa Serikali, Wizara ya Afya, hospitali za umma na binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya afya waliojitolea kusogeza huduma karibu na wananchi bila kuwatoza gharama.

Aidha, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika huduma za afya nchini, huku akitoa shukrani kwa madaktari, wauguzi na wataalamu wote wanaoshiriki kuhakikisha wananchi wa Arusha wanapata huduma bora kupitia kambi hiyo ya matibabu bila malipo.