Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas,akizungumza na wadau wa sekta ya maji kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.

Diwani wa Kata ya Shule ya Tanga Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Febronia Tindwa,akitoa maoni ya mapendekezo mapya ya bei za huduma za maji wakati wa kikao cha kukusanya maoni ya wadau kilichohitishwa na Mamlaka ya Udhibiti.

Baadhi ya wadau wa sekta ya maji Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa huo Brigedia Jenerali Ahmed Abbas(hayupo Pchani)wakati akifungua kikao cha wadau Kwa ajili ya kupata maoni huu ya marekebisho ya bei za huduma za maji zilizotolewa na Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira(Souwasa)

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura Walter Christopha,akizungumza kwenye kikao cha wadau wa sekta ya Maji.
Picha no 293 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa)Mhandisi Rejea Samwel akitoa ufafanuzi wa hoja za wadau wa maji.
……………
Na Mwandishi Wetu, Songea
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA)kanda za nyanda za juu kusini,imekutana na wadau wa maji wa Manispaa ya Songea ili kupata maoni kuhusu marekebisho ya bei za huduma za maji yaliyowasilishwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa mazingira Manispaa ya Songea(Souwasa).
Akizungumza katika kikao cha wadau kilichofanyika mjini Songea,Mkurugenzi wa ufundi wa Souwasa Jafari Kinjalambaya amesema,hatua hiyo inalenga kuiwezesha mamlaka kuendelea kutoa huduma bora,salama na endelevu kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto ya ongezeko la gharama za uendeshaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira.
Kinjalambaya ametaja viwango vipya vilivyopendekezwa na Souwasa kwa mwaka wa fedha 2026/2027,wateja wa majumbani wanaotumia zaidi ya mita za ujazo tano kwa mwezi watalipa 2,700 kutoka Sh.1,730 ya mwaka 2025/2026,taasisi zitalipa Sh.2,750 badala ya Sh.1,780.
“Kwa sehemu za biashara bei ya huduma ya maji tuliyopendekeza ni Sh.2,800 kutoka Sh.1,820 ya awali,kwa watu wenye viwanda tumependekeza bei ya Sh.2,800 badala ya Sh.1,820 na magati(vituo vya kuchotea maji) Sh.1,500 ambayo ni ongezeko la Sh.1,000 ya awali”alisema Kinjalambaya.
Alisema, marekebisho hayo yatasaidia kuimarisha upatikanaji wa majisafi, kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa maji,kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wateja na kuwezesha utekelezaji wa miradi mipya ya upanuzi wa huduma katika maeneo yanayohudumiwa na Souwasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Mhandisi Rejea Samwel Ng’ondya alisema,Souwasa itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji wa miji 28 ili kuhakikisha wanatoa huduma bora ya maji kwa wananchi wa Manispaa ya Songea.
“Naomba niwatie moyo wadau wetu,baada ya muda mfupi mambo yatakuwa mazuri kwani Mkandarasi yupo saiti anaendelea na ujenzi wa mradi na tunatarajia muda wowote ataanza ujenzi wa chujio ili kumaliza kero ya kupata maji machafu”alisema Ng’ondya.
Alisema, majisafi na salama ni hitaji muhimu kwa maisha ya binadamu,afya ya jamii,maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa mazingira,hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha miundombinu ya maji inalindwa,inaboreshwa ili wananchi wengi waweze kunufaika na huduma hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas, ameipongeza Souwasa kwa juhudi zake za kuendelea kuboresha huduma za maji na kukutana na wadau kwa ajili ya kupitia mchakato wa mapendekezo ya huduma za bei za maji.
Alisema,utaratibu huo unaonyesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha maamuzi yanayohusu huduma za umma yanazingatia ushirikishwaji wananchi na wadau mbalimbali kabla ya kufanyika maamuzi ya mwisho.
Alisema, mkoa wa Ruvuma umeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu upanuzi wa maeneo ya makazi na shughuli za kiuchumi,zinazokwenda sambamba na kuongezeka mahitaji makubwa ya huduma za majisafi na salama.
Alisema, sekta ya maji ni muhimu kwani inayogusa maisha ya kila siku ya wananchi na kuchangia maendeleo ya kijamii,kiuchumi ya Taifa lolote,hivyo huduma ya majisafi na salama ni msingi wa afya bora ustawi wa jamii na ukuaji wa shughuli za uzalishaji na sekta nyingine ikiwemo elimu,afya,viwanda na biashara.
Alisema, ndiyo maana Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya maji kwa lengo la kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inawafikia wananchi wengi zaidi na itaendelea kusogeza huduma za maji kwa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Ewura Mhandisi Walter Christopha alisema,mkutano huo ni sehemu ya uchunguzi wa Ewura kupata maoni ya wadau kabla ya kutoa maamuzi kuhusu maombi ya kurekebisha bei za huduma za majisafi na usafi wa mazingira yaliyowasilishwa na Souwasa.
Alisema, maoni ya wadau yanasaidia kufikia uamuzi wa haki kuhusu maombi ya Souwasa kama ilivyofanya mwaka 2022 ambapo wadau walikubali maombi ya Souwasa kupandisha bei ya huduma za maji.
Diwani wa kata ya Shule ya Tanga Febronia Tindwa alisema,bei ya huduma za maji iliyopendekezwa na Souwasa ni rafiki kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji,lakini ameshauri ongezeko hilo liende sambamba na kuboresha huduma za maji kwa wananchi ili kumaliza changamoto ya upatijanaji wa maji kwa mgao.
