NA DENIS MLOWE, IRINGA.
MKOA wa Iringa umeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030 baada ya kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato, kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, mbele ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Iringa na kufanyika katika ukumbi wa CCM mkoani akisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa Serikali za Mitaa na wananchi.
Kheri alisema mkoa umeendelea kutekeleza vipaumbele vya ilani vinavyolenga kupunguza umaskini, kuimarisha kilimo, mifugo na uvuvi, kukuza viwanda, kuongeza upatikanaji wa umeme, kuimarisha sekta ya utalii, kuboresha elimu, afya, maji, miundombinu na kuwezesha wanawake, vijana pamoja na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Alisema katika kipindi hicho Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa ilikusanya zaidi ya shilingi bilioni 72, huku ikiendelea kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa miaka mitano mfululizo.
Aliwapongeza wafanyabiashara, walipakodi na wananchi kwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi, akieleza kuwa mafanikio hayo yameongeza uwezo wa Serikali kugharamia huduma muhimu za maendeleo.
Kwa upande wa halmashauri, alisema zimekusanya zaidi ya shilingi bilioni 39 za mapato ya ndani, huku Halmashauri ya Mji wa Mafinga ikiongoza kwa kuvuka lengo lake kwa zaidi ya asilimia 115.
Aidha, alisema Serikali ilielekeza zaidi ya shilingi bilioni 287 kupitia halmashauri na taasisi mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji, barabara, kilimo na huduma nyingine za kijamii.
Katika sekta ya afya, Kheri alisema Serikali imeendelea kujenga na kuboresha hospitali, vituo vya afya na zahanati pamoja na kuajiri watumishi wapya 423 wa kada mbalimbali ili kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.
Alisema miradi ya afya yenye thamani ya mabilioni ya shilingi inaendelea kutekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu, wadau wa maendeleo na mapato ya ndani ya halmashauri, huku baadhi ikiwa imekamilika na mingine ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Akizungumzia sekta ya elimu, Kheri alisema mkoa umeendelea kujenga madarasa, mabweni, nyumba za walimu, maabara, maktaba na miundombinu mingine ya shule kupitia fedha za Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Aliongeza kuwa zaidi ya asilimia 98 ya shule za msingi na shule zote za sekondari za Serikali zimeendelea kutekeleza mpango wa chakula shuleni, hatua inayochangia kuongeza mahudhurio ya wanafunzi, kuboresha ufaulu na kupunguza utapiamlo.
Katika sekta ya maji, alisema IRUWASA inaendelea kutekeleza miradi 16 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 39 katika wilaya za Kilolo, Iringa na Mufindi, huku baadhi ya miradi ikiwa tayari imeanza kutoa huduma na mingine ikiwa katika hatua za mwisho za kukamilika.
Kwa upande wa miundombinu, alisema TARURA na TANROADS zinaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege, hatua inayorahisisha usafiri, biashara na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kheri alisema Serikali pia imeendelea kuimarisha sekta za ardhi, umwagiliaji, kilimo na uwekezaji kupitia upimaji wa viwanja, utoaji wa hatimiliki, utatuzi wa migogoro ya ardhi na utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.
Alisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa miradi umechangia kukamilika kwa miradi mingi kwa wakati na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa ilani ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na matunda ya maendeleo katika sekta zote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, alisema Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa ilifanya ziara katika wilaya zote za mkoa huo na kujiridhisha kuwa miradi mingi inayotekelezwa chini ya ilani imefikia hatua nzuri na inaendelea kuwanufaisha wananchi.
Alisema kamati hiyo ilikagua miradi mbalimbali ikiwemo shule mpya za sekondari, Chuo cha VETA Kilolo pamoja na mradi wa uzalishaji wa hewa tiba (Medical Oxygen) wilayani Mufindi, ambao umefikia hatua za mwisho za utekelezaji na unatarajiwa kuanza kutoa huduma hivi karibuni.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, aliipongeza Serikali kwa mafanikio yaliyopatikana lakini akaomba kuwepo kwa mpango wa kuboresha maeneo ya kuingilia mkoa huo ili yawe na mandhari yanayoendana na hadhi ya Iringa kama kitovu cha utalii na biashara.
Ngajilo pia alisisitiza umuhimu wa kurejeshwa kwa timu ya ligi kubwa mkoani Iringa akieleza kuwa hatua hiyo itachochea maendeleo ya michezo, biashara na shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Naye Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga, aliitaka Serikali kuendelea kushirikiana kwa karibu na wabunge katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hususan ukarabati wa shule kongwe za msingi, uboreshaji wa barabara za vijijini, upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kuongeza watumishi katika sekta za elimu na afya.
Kiswaga alisema pia kuna haja ya kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu fidia, matumizi ya nishati pamoja na miradi ya maendeleo ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika utekelezaji wa mipango ya Serikali.
Kwa ujumla, viongozi hao walieleza kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM Mkoa wa Iringa unaendelea kuzaa matunda kupitia miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi, huku wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kushughulikia changamoto zilizobaki ili kuharakisha maendeleo ya mkoa wa Iringa.