Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Ngeleja Kadonya, amewasihi watendaji wa Idara na vitengo vinavyoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki kuendelea kufanya kazi kwa umoja, uwajibikaji na weledi ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na msimamo imara katika masuala ya kikanda na kulinda maslahi ya taifa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza katika kikao chake na watumishi wa Idara hiyo kilichofanyika Mtumba, Jijini Dodoma, Julai 16, 2026, Katibu Mkuu amesisitiza kuwa mchango wa kila mtendaji ni muhimu katika maandalizi ya msimamo wa nchi (country position) unaowasilishwa katika vikao mbalimbali vya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hivyo, watendaji watambue wajibu wao katika kufanikisha malengo ya taifa.
Ameeleza kuwa masuala ya ushirikiano wa kikanda yanahitaji maandalizi makini, uratibu mzuri na ushirikiano wa karibu kati ya watendaji wa idara mbalimbali. Amewataka watendaji kufanya kazi kama timu moja, kwa kuzingatia maelekezo ya viongozi wakuu na kuhakikisha majukumu yanatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyotarajiwa.
“Tunapaswa kuelewa kuwa kila mmoja wetu ana nafasi katika kujenga msimamo wa nchi. Tunaposhiriki katika majadiliano ya kikanda, tunawakilisha maslahi ya Tanzania, hivyo maandalizi yetu lazima yawe thabiti na yenye ubora,” alisema.
Katibu Mkuu pia amesisitiza umuhimu wa kuandaa na kusambaza taarifa za mrejesho (Back to Office Reports) baada ya watendaji kushiriki katika vikao na shughuli mbalimbali za kikazi.
Katika kikao hicho, watendaji walipata fursa ya kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha utendaji wa idara. Walisisitiza umuhimu wa kuimarisha uratibu wa ndani, kuboresha mifumo ya mawasiliano na kuhakikisha taarifa muhimu zinawafikia wahusika kwa wakati.
Akijibu hoja hizo, Katibu Mkuu aliwahimiza watendaji kutumia fursa ya sera yake ya mlango wazi (Open Door Policy) kuwasilisha mawazo, changamoto na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utendaji wa taasisi.
“Hatuna taasisi isiyokumbana na changamoto,Muhimu ni kuwa na utamaduni wa kuzungumza, kutafuta suluhisho na kufanya maboresho pale yanapohitajika,” alisisitiza.
Akihitimisha kikao hicho, Katibu Mkuu aliwashukuru watumishi kwa ushiriki wao na mchango walioutoa katika majadiliano, akieleza kuwa kikao hicho kimetoa fursa ya kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha mshikamano wa kikazi.

