Na John Mapepele- Dodoma

Serikali imeeleza dhamira yake ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za afya za kibingwa katika Afrika Mashariki na Kati huku ikitoa wito kwa Watanzania na wadau mbalimbali kushiriki kuchangia Mfuko wa Upandikizaji wa Figo na Uloto ili kuwawezesha wagonjwa wasiokuwa na uwezo kupata matibabu yanayookoa maisha.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa (Mb), wakati akiwasilisha taarifa kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), katika hafla ya chakula cha pamoja cha kuchangisha fedha kwa ajili ya kugharamia huduma za upandikizaji wa figo na uloto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, iliyofanyika jijini Dodoma.

Akizungumza mbele ya viongozi wa Serikali, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), viongozi wa dini, wadau wa sekta ya afya na wageni mbalimbali,

Waziri Mchengerwa alisema hafla hiyo haikulenga chakula pekee, bali ilikuwa ni juhudi za kuokoa maisha ya Watanzania wanaohitaji matibabu ya kibingwa.

Alisisitiza kuwa kila mchango utakaotolewa utakuwa sehemu ya kuwapa wagonjwa nafasi mpya ya kuishi, akieleza kuwa historia ya taifa itaikumbuka siku hiyo kama mwanzo wa hatua muhimu katika safari ya Tanzania kujitegemea katika huduma za tiba za kibingwa.

Waziri Mchengerwa aliipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka kumi tangu kuanzishwa kwake. 

Alisema hospitali hiyo imekua kutoka kuwa wazo hadi kuwa kituo cha kisasa kinachotoa huduma za ubingwa 20 na ubingwa bobezi 17 kwa kutumia wataalamu waliobobea pamoja na teknolojia za kisasa.

Alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuifanya sekta ya afya kuwa miongoni mwa vipaumbele vya maendeleo ya taifa.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hadi sasa wagonjwa 58 wamefanyiwa kwa mafanikio upandikizaji wa figo nchini, huku watoto 31 wenye ugonjwa wa selimundu wakifanyiwa upandikizaji wa uloto

Alisema mafanikio hayo si takwimu pekee bali yanawakilisha maisha ya wananchi waliorejeshewa matumaini, familia zilizookolewa dhidi ya majonzi, na watoto waliorejea shuleni baada ya kupata matibabu yaliyokuwa yakipatikana nje ya nchi pekee.

Aidha, alisema huduma hizo zimeokoa mabilioni ya shilingi ambayo hapo awali yalikuwa yanatumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu, hatua iliyoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazotoa huduma hizo za kibingwa.

Waziri Mchengerwa aliipongeza Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa kuandaa hafla hiyo ya kuchangisha fedha, akieleza kuwa wanawake wamekuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya sekta ya afya na ustawi wa familia nchini.

Alisema wanawake wamekuwa wakibeba jukumu kubwa la kuwahudumia wagonjwa majumbani, kuwapeleka watoto hospitalini na kugharamia matibabu kwa kujitolea, hivyo mchango wa UWT katika kuanzisha kampeni ya kitaifa ya kusaidia wagonjwa wa figo na uloto ni mwendelezo wa jukumu ambalo wanawake wamekuwa wakilitekeleza kwa miaka mingi.

Serikali kuanzisha vituo vya umahiri

Waziri wa Afya alisema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji wa Figo kwa kushirikiana na TOKUSHUKAI Medical Corporation ya Japan.

Pia alisema maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Afrika Mashariki cha Upandikizaji wa Uloto na Sayansi ya Magonjwa ya Damu pamoja na kukamilisha Kituo cha Saratani katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Alifafanua kuwa miradi hiyo inalenga kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za afya, mafunzo, tafiti na tiba utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Waziri Mchengerwa alisema bado zipo familia nyingi zinazoshindwa kumudu gharama za upandikizaji wa figo na uloto, jambo linalowafanya baadhi ya wagonjwa kushindwa kupata huduma licha ya uwepo wa wataalamu na vifaa vya kisasa. 

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wadau wa maendeleo, taasisi za umma na binafsi, makampuni, mashirika ya dini, wafanyabiashara na wananchi wote kuendelea kuchangia Mfuko wa Upandikizaji wa Figo na Uloto ili kuhakikisha kila mgonjwa anayehitaji huduma hiyo anapata nafasi ya kutibiwa bila kujali uwezo wake wa kifedha.

Waziri Mchengerwa alimshukuru Waziri Mkuu kwa kushiriki hafla hiyo pamoja na kuipongeza Menejimenti, Bodi na watumishi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa juhudi zao za kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.

Pia aliwapongeza viongozi na wanachama wa UWT kwa kuandaa hafla hiyo yenye lengo la kuokoa maisha ya Watanzania wengi, akisisitiza kuwa mshikamano wa wananchi utawezesha wagonjwa wengi zaidi kupata huduma za upandikizaji wa figo na uloto.

Alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kushiriki katika jitihada za kuokoa maisha ya wenzao, akisisitiza kuwa historia haitawakumbuka kwa kile walichokula siku hiyo, bali kwa maisha waliyosaidia kuyaokoa kupitia michango yao.