
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini Mahwaya (kulia) akitoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia leo, Julai 16, 2026, Kigamboni, Dar es Salaam

Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Wilaya ya Mikwambe, Godwin Marandu (wa kwanza kushoto) akitoa elimu kwa wananchi kuhusu kutumia huduma za kidijitali za TANESCO, ikiwemo Luku Kijanja, MCHONGO 180 na NIKONEKT JISOTI, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza ufanisi.

………………
Katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Kigamboni limetoa elimu kwa wananchi wa Soko la Tungi Mnadani, Kigamboni, Dar es Salaam, kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza leo, Julai 16, 2026, wakati akitoa elimu hiyo, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini Mahwaya, amesema lengo ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za kutumia ya umeme kwa ajili ya kupikia, kwani ni salama, wenye gharama nafuu na rafiki kwa mazingira.
Bi. Mahwaya amewahamasisha wananchi kutumia matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia umeme, akieleza kuwa huokoa muda wa kupika, hulinda afya kwa kutotoa moshi, huboresha usafi wa mazingira na hutumia kiwango kidogo cha umeme.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutumia majiko sanifu ya umeme yanayotumia teknolojia ya kisasa na rafiki ili kuongeza ufanisi na kuboresha maisha ya wananchi.
“Ni wakati kwa wananchi wetu kutambua kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yana faida nyingi, ikiwemo gharama nafuu, kuokoa muda wa kupika na, zaidi ya yote, kulinda mazingira yetu. TANESCO itaendelea kutoa elimu ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanatumia majiko haya majumbani,” amesema Bi. Mahwaya.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Wilaya ya Mikwambe, Godwin Marandu, amewahimiza wananchi kutumia huduma za kidijitali za TANESCO, ikiwemo Luku Kijanja, MCHONGO 180 na NIKONEKT JISOTI, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza ufanisi.
Baadhi ya wananchi waliopata elimu hiyo wameishukuru TANESCO kwa kuwapatia uelewa kuhusu matumizi ya majiko sanifu ya umeme, wakieleza kuwa majiko hayo hutumia umeme kidogo pamoja na kupunguza gharama za matumizi ya nishati.
