NA DENIS MLOWE,IRINGA
MKUU.wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema maonesho ya Nanenane yanayofanyika kwa mara ya kwanza ndani ya Mkoa wa Iringa yanalenga kusogeza huduma kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili wapate fursa ya kujifunza teknolojia za kisasa, kuongeza tija katika uzalishaji na kuunganishwa na masoko.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo katika Viwanja vya Utalii Kihesa Kilolo,Kheri alisema hatua ya kuandaa maonesho hayo Iringa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi badala ya kuwalazimu kusafiri umbali mrefu kufuata maonesho ya kanda.
Alisema maendeleo ya sekta ya kilimo hayawezi kupatikana kwa kuongeza uzalishaji pekee, bali yanahitaji matumizi ya teknolojia za kisasa, ubunifu, uwekezaji, ushirikiano kati ya wadau pamoja na upatikanaji wa masoko yenye uhakika.
Kheri alisema Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa inayoongoza nchini kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kutokana na ardhi yenye rutuba, hali nzuri ya hewa na rasilimali za maji, huku mwaka 2023 ukizalisha zaidi ya tani milioni moja za mazao ya chakula na tani 137,888 za mazao ya biashara.
Alisema bado ipo haja ya kuongeza tija kwa kutumia mbegu bora, pembejeo sahihi, kilimo cha kisasa, umwagiliaji, teknolojia za kisasa za uzalishaji, uhifadhi na uchakataji wa mazao ili kuongeza kipato cha wakulima.
Aidha alisema kuwa changamoto nyingine ni wakulima wengi kuzalisha bila kuzingatia mahitaji ya soko, hali inayosababisha kushuka kwa bei za mazao na kupunguza faida kwa wazalishaji. 
James Alisisitiza umuhimu wa wakulima kuzingatia taarifa za soko kabla ya kuanza uzalishaji na kuongeza kuwa maonyesho hayo yatakuwa ya kila mwaka na upande wa manispaa wataratibu kwa miaka mitatu mfululizo na kwenda halmashauri nyingine za mkoa.
Aidha aliwataka wananchi kutumia fursa zinazotokana na kukua kwa sekta ya utalii mkoani Iringa kwa kuzalisha mazao yanayohitajika na hoteli na maeneo ya utalii, ikiwemo mboga mboga, badala ya kutegemea mazao ya kawaida pekee.
Aliwahimiza pia wakazi wa Manispaa ya Iringa kutumia maeneo madogo yaliyopo katika makazi yao kwa kilimo cha bustani ili kupunguza gharama za maisha na kuongeza kipato cha familia kupitia uzalishaji wa mboga, matunda na mazao mengine ya muda mfupi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa anayeshughulikia Uchumi na Sekta za Uzalishaji, Elia Luvanda, alisema maonesho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Tambua Soko, Ongeza Tija, Tekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
Alisema jumla ya washiriki 87 wameshiriki maonesho hayo wakiwemo halmashauri zote za Mkoa wa Iringa, taasisi za utafiti, kampuni za mbegu na pembejeo, taasisi za fedha, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo wanaohudumia sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Naye Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, alisema maonesho hayo yanafungua fursa mpya za biashara kwa wananchi na kuongeza shughuli za kiuchumi ndani ya manispaa, huku akieleza matarajio ya kuona tukio hilo likiendelea kufanyika kila mwaka.
Na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, alisema maonesho hayo yanapaswa kuwa chachu ya kupeleka teknolojia na maarifa yaliyooneshwa kwa wananchi ili yaweze kuleta mabadiliko halisi katika uzalishaji na uchumi wa wakulima wa Mkoa wa Iringa.