Na Jeremia Mwakyoma, Picha na Gladys Lukindo

DODOMA – JULAI 15, 2026

Awamu ya pili ya watoto kutoka nchini Burundi, kesho wanatarajiwa kuwasili nchini kwa ajili ya matibabu ya upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH).

Balozi wa Tanzania nchini Burundi Mhe. Gelasius Byakanwa ameyasema hayo wakati alipotembelea BMH kuwajulia hali watoto kutoka Burundi waliokuja awamu ya kwanza ambao tayari wameshafanyiwa upasuaji wa moyo na Afya zao zimeimarika.

“Serikali imefanya kazi kubwa ya kuwekeza miundombinu na vifaa tiba vya kisasa kama ilivyo kwa BMH na kuendeleza rasilimali watu kiasi cha kuzalisha Madaktari Bingwa wabobezi kiasi cha nchi zinazotuzunguka kuamini wanaweza kupata huduma za ubobezi hapa Tanzania badala ya kuwaza kwenda nchi za mbali” alisisitiza Balozi Byakanwa.

Balozi Byakanwa aliahidi ofisi yake itasaidia mwaka huu wa fedha kuweza kufanya kambi nyingine ya matibabu nchini Burundi au kliniki maalumu ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kutoka Burundi kufuata huduma za Tiba Utalii hapo BMH lengo kuifanya BMH kuwa kitovu cha Tiba Utalii kwa nchi zinazozunguka Tanzania.

Aidha, amepongeza timu za wataalamu na uongozi wa Hospitali za BMH na JKCI kwa kutoa matibabu yenye ubora kwa watoto waliokuja awali kutoka Burundi na wadau waliofadhili gharama za watoto hao kutoka Burundi kuja kutibiwa BMH.

 Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amepongeza falsafa ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ya kufanya “Reforms” kwenye Diplomasia ya Afya na kumpongeza Balozi Byakanwa kwa kusimamia utekelezaji wake huku akiahidi BMH ipo tayari kuwahudumia Tiba Utalii Wananchi kutoka nchi nyingine kwenye maeneo ya moyo, saratani, upandikizaji viungo na matatizo ya mfumo wa mkojo.

Nae Bw. Shedrack Nzigiyimana akiwakilisha Wazazi ambao watoto wao tayari wamefanyiwa upasuaji wa moyo, amemjulisha Mhe Balozi kuwa, tangu wamewasili BMH wamepokelewa kwa ukarimu, wamepewa huduma za kiwango cha juu ambazo zimesaidia watoto wao kurejea kwenye Afya njema baada ya kukamilisha upasuaji.