Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, Bw. Innocent Rwetabura akizungumza katika. mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam Julai 16, 2026.

………….

Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imesema imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 1.2 katika kipindi cha miaka minne iliyopita ili kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kuhakikisha teknolojia za kisasa za 4G na 5G zinawafikia wananchi katika kila kona ya Tanzania.

Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha urithi wa Hayati Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, Bw. Innocent Rwetabura, amesema uwekezaji huo umechangia kuharakisha mageuzi ya kidijitali nchini, hususan katika sekta ya afya kupitia matumizi ya teknolojia.

“Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Yas imewekeza zaidi ya shilingi trilioni 1.2 kuhakikisha teknolojia za kisasa, ikiwemo mtandao wa 4G na 5G, zinapatikana katika kila kona ya Tanzania. Tunaamini uwekezaji huu unachangia kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, ikiwemo huduma za afya kupitia suluhisho za kidijitali,” amesema Rwetabura.

Amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaipa teknolojia nafasi muhimu katika kuimarisha mifumo ya afya kupitia taarifa sahihi za afya, suluhisho za afya kidijitali na kufanya maamuzi yanayotegemea takwimu.

Kwa mujibu wa Rwetabura, uwekezaji wa Yas umewezesha kupanuka kwa huduma mbalimbali za afya za kidijitali ikiwemo tiba kwa njia ya mtandao (telemedicine), uchunguzi wa magonjwa kwa njia za kidijitali, mafunzo endelevu kwa wataalamu wa afya pamoja na kuboresha huduma za dharura zinazowafikia wananchi kwa haraka zaidi.

Aidha, alisema Yas imeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali katika kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii.

Kupitia ushirikiano kati ya Yas, Serikali kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na UNICEF, zaidi ya watoto milioni 13 wenye umri chini ya miaka mitano wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa kwa kutumia teknolojia ya simu kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS).

Vilevile, Yas imeshirikiana na Hospitali ya CCBRT kuwezesha matibabu kwa watoto wenye tatizo la miguu ya kupinda (clubfoot), huku ikiendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya macho bure Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo zaidi ya Watanzania 23,000 tayari wamenufaika.

Rwetabura amesema Yas pia ipo katika mazungumzo na Taasisi ya Benjamin William Mkapa kwa lengo la kuanzisha ushirikiano wa kimkakati utakaosaidia kuendeleza miradi endelevu ya afya na maendeleo kwa wanawake, watoto na vijana Tanzania Bara na Zanzibar.

“Tutaendelea kuwekeza katika teknolojia bunifu na miundombinu ya mawasiliano ili kuimarisha mifumo ya afya, kuwawezesha vijana kuleta ubunifu katika sekta ya afya na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga Tanzania yenye huduma bora za afya na maendeleo jumuishi,” amesema Rwetabura.