Na John Walter -Mbulu
Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara imeupokea rasmi Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 katika Kata ya Gehandu, ukitokea Halmashauri ya Mji wa Babati, ambapo utakagua, kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi 15 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 50.9.
Akiupokea Mwenge huo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Babati, Remidius Mwema, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu, amesema Mwenge wa Uhuru utapitia miradi 15 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 50.9, ambayo imegusa sekta mbalimbali ikiwemo maji, afya, elimu, miundombinu na uwezeshaji wa wananchi.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, amewahimiza wananchi wa Mbulu kuendelea kuilinda na kuitunza amani ya Tanzania, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.
Amesema kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 isemayo, “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo,” inapaswa kuwa chachu ya kuimarisha mshikamano, uwajibikaji na ushirikiano wa wananchi katika kuchochea maendeleo ya nchi.
Aidha, Mwang’onda amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa, UKIMWI na malaria, pamoja na kuzingatia lishe bora kwa watoto na familia kwa ujumla ili kujenga jamii yenye afya na nguvu kazi yenye tija.
Amesisitiza kuwa Mwenge wa Uhuru unaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuhamasisha maendeleo, uwajibikaji na mshikamano wa Watanzania, huku ukitoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii yanayogusa ustawi wa taifa.

