Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENGE wa uhuru umetembelea na kukagua mradi wa maji wa thamani ya shilingi bilioni 4.3 utakaonufaisha watu 57000 wa Tarafa ya Moipo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Kaimu Mkurugenzi wa mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Arusha (AUWSA) Kazimili Kanyanza ameeleza hayo akisoma taarifa ya mradi huo baada ya mwenge wa uhuru kutembelea na kukagua mradi huo wa maji.
Kanyanza ameeleza kwamba watu 57,000 wakazi wa Tarafa ya Moipo wa kata za Mirerani, Endiamtu, Naisinyai na Shambarai, watanufaika na mradi huo.
Amesema fedha za mradi huo shilingi bilioni 4.3 zimetoka Serikali na hadi hivi sasa zimetumika kiasi cha shilingi bilioni 2.5 katika ujenzi wa mradi huo.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 Wazo Mwang’onda ameipongeza mamlaka hiyo ya AUWSA kwa kufikisha hatua hiyo mradi huo.
“Mradi huu ukikamilika lile lengo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan la kumtua ndoo mama kichwani litatimia maana maji yatakuwa mwaaa mwaaa kila mahali, asante sana,” amesema Mwang’onda.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki James Ole Millya ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro amesema mradi huo ukikamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii ya eneo hilo la Tarafa ya Moipo.
“Mama yetu mpendwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tunamshukuru sana anaendelea kutukumbuka kwenye maendeleo hasa kwenye maji na pia kwa mara ya kwanza Wilaya ya Simanjiro imepata kijana ambaye ni Naibu Waziri tunasema asante sana,” amesema Ole Millya.
