Na Atley Kuni, WAF – Dodoma
Wizara ya Afya imeendelea kuwekeza uimarishaji wa rasilimali watu kwa kuwajengea uwezo wakufunzi wa vyuo vya kati na vya juu vya afya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha ubora wa elimu ya afya nchini na kuandaa wataalamu Afya wenye ujuzi unaoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yamebainisha wakati wa mafunzo kwa wakufunzi 13 wa Dodoma Institute of Health and Allied Sciences (DIHAS) yanayofanyika leo Julai 15, 2026, katika Chuo cha Mirembe jijini Dodoma.
Mratibu wa Mafunzo Kazini kutoka Wizara ya Afya, Bi. Notgera Ngaponda, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wakufunzi ili waendelee kutumia mbinu za kisasa za ufundishaji na kutoa maarifa yanayokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.
Amesema tathmini iliyofanyika katika baadhi ya vyuo vya afya nchini ilibaini uwepo wa mapungufu katika eneo la mafunzo ya Afya ya Uzazi, jambo lililoifanya Wizara kuandaa mpango wa kuwafikia wakufunzi zaidi ya 450 kutoka vyuo 47 vya afya nchini.
“Utafiti wa mwaka 2025, ulitoa mapendekezo ya namna ya kuwawezesha wakufunzi wetu kuendana na mabadiliko yanayoendelea duniani. Lengo ni kuhakikisha wanakwenda na mahitaji ya wakati,” amesema Bi. Ngaponda.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayosisitiza uimarishaji wa rasilimali watu katika sekta ya afya pamoja na kuboresha huduma za afya ya mama, mtoto na uzazi kwa ujumla. Aidha, amewataka washiriki kuyatumia kikamilifu mafunzo hayo ili maarifa watakayoyapata yawe chachu ya kuboresha ufundishaji kwa wanafunzi wao.
Kwa upande wao, wakufunzi walioshiriki akiwepo Bi. Latifa Mtitu, na Bw. Gitinkwi, wamesema taaluma ya afya ni eneo linalobadilika kila wakati kutokana na maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia, hivyo mafunzo endelevu ni muhimu ili kuhakikisha wakufunzi na wanafunzi wanapata maarifa sahihi na ya kisasa.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuchangia kuimarisha uwezo wa wakufunzi, kuongeza ubora wa elimu ya afya na kuzalisha wataalamu wenye ujuzi kuelekea dira 2050.

