………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Miradi ya usambazaji umeme vijijini(REA) imeipaisha Tanzania kidunia ambapo inashika nafasi ya kwanza Afrika kwa kupeleka umeme kwenye maeneo hayo kwa asilimia 75.2.
Waziri wa Nishati Dk.Medard Kalemani amesema hayo wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge bungeni zilizoibuka wakati wa kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2020/21,
Kalemani amesema miradi hiyo imeipa sifa kubwa Tanzania na kuishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo kupeleka umeme kwa watanzania.
“Takribani Sh.Trilioni 2.8 zimetumika kuwapelekea umeme wananchi kwenye maeneo haya, huwezi kuzungumza viwanda kama umeme vijijini haupo, maeneo ya viwanda yapo vijijini ndio maana umeme umepelekwa huko,”ameeleza Kalemani.
Amebainisha Kalemani kuwa mwaka 2008 Tanzania ilipoanza kutekeleza miradi ya REA ilishika nafasi ya 50 Afrika na kuwa na asilimia 16.5.
“Mwaka 2015 tulifikisha asilimia 39.6 na kushika nafasi ya 25 Afrika, mwaka 2017 tulifikia asilimia 47 na kushika nafasi ya 18, mwaka 2018 tulifikia nafasi ya nne Afrika tukiwa na asilimia 58,”amesema Kalemani.
Hata hivyo katika hatua nyingine amesema mwaka 2019 ilishika nafasi ya tatu huku Afrika kusini walikuwa na asilimia 64 na Nigeria asilimia 72.
“Mwaka huu 2020 mwezi wa Februari tumeshika namba moja Afrika kwa asilimia 75.2, nipongeze sana serikali kwa kutoa fedha za kupeleka umeme kwa wananchi wake, niwapongeze pia wabunge kwa ushirikiano,”ameongezea Kalemani.
Aidha amesema kuwa Wilaya 35 kata na vijiji vyote vimefikiwa na umeme na kwamba mradi ujao umeme utapelekwa kwenye vitongoji.
Waziri huyo amesema hatua iliyofikiwa hivi sasa zimetengwa tani milioni 10 za gesi asilia kwa ajili ya kutekeleza mradi huku ikitenga fedha ya kuwalipa fidia wananchi 693 wenye hekari takribani 2,071.
Akizungumza kuhusu mradi wa bomba la mafuta, Kalemani alisem imeshafanyika tathmini ya watu wanaopaswa kufidiwa ambapo watu 9,000 kwa upande wa eneo linapopita bomba na watu 3,420 kwenye maeneo zitakapojengwa camp.
Kwa kuhitimisha Sh.Bilioni 50 zimetengwa na serikali na zilishapitishwa na Bunge huku akisisitiza kuwa miradi hiyo itatekelezwa kama ilivyopangwa na vikao kati ya Tanzania na Uganda vinafanyika kwa njia ya mtandao kutokana na janga la Corona.