Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, amesema shirika hilo linaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati itakayoongeza upatikanaji wa umeme Zanzibar, huku likiharakisha utekelezaji wa mpango wa nishati safi ya kupikia na kuanzisha teknolojia mpya zitakazoboresha huduma kwa wateja.
Bw. Twange ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kutembelea banda la TANESCO katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Amesema moja ya maeneo waliyomueleza Rais Dkt. Mwinyi ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa nishati safi ya kupikia, ambapo TANESCO imeanzisha mpango wa Bill Financing unaowawezesha wateja wapya na waliopo kukopeshwa majiko ya umeme na kulipa gharama zake kidogo kidogo kupitia ununuzi wa umeme.
“Mpango huu umekuwa na mwitikio mzuri sana. Mafanikio yake ni zaidi ya asilimia 90. Tayari tumeingia makubaliano na wadau wa sekta binafsi na tumeanza kukopesha majiko kwa wananchi. Tunatoa wito kwa wananchi wasiogope kutumia umeme kwa kupikia kwa sababu ni nishati nafuu, salama na rafiki kwa mazingira,” amesema Bw. Twange.
Ameongeza kuwa kupitia mradi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 282, TANESCO imetenga dola milioni sita kwa ajili ya kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia umeme, mradi unaotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).
Akizungumzia upatikanaji wa umeme Zanzibar, Bw. Twange amesema TANESCO inaendelea na maandalizi ya mradi mkubwa wa kujenga njia mpya za kusafirisha umeme kupitia nyaya zinazopita chini ya bahari, ambapo kutakuwa na njia kutoka Dar es Salaam kwenda Unguja, Tanga kwenda Pemba na Kisiju kwenda Mafia.
Amesema mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), huku mshauri elekezi akitarajiwa kupatikana mwezi Agosti na mkandarasi mwezi Januari, ambapo utekelezaji wake utachukua miezi 22.
“Mahitaji ya umeme Zanzibar yameongezeka kutokana na kasi ya maendeleo, hususan katika sekta za utalii, uwekezaji, ujenzi wa hoteli, shule na hospitali. Mradi huu utaongeza uwezo wa kusafirisha umeme na kuhakikisha huduma inakuwa ya uhakika zaidi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Bw. Twange amesema TANESCO imeanza kuandaa teknolojia mpya ya Smart House, ambayo itawawezesha wateja kufuatilia matumizi ya umeme kupitia simu zao za mkononi.
Amefafanua kuwa mfumo huo utamruhusu mteja kuona kifaa kinachotumia umeme mwingi ndani ya nyumba na hata kukizima akiwa mbali na nyumbani, hatua ambayo itasaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuondoa malalamiko kuhusu matumizi makubwa ya umeme.
“Tunataka kutumia teknolojia kupunguza usumbufu kwa wateja wetu. Kila changamoto wanayotuletea tunaichukua kama fursa ya kuboresha huduma na kutafuta suluhisho la kudumu,” amesema.
Aidha, amesema TANESCO inaendelea kuhamasisha matumizi ya umeme katika sekta ya usafiri kupitia magari, pikipiki na bajaji za umeme, huku ikiendelea kujenga vituo vya kuchaji magari hayo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika uzalishaji wa umeme, ikiwemo kupitia Bwawa la Julius Nyerere, unapaswa kwenda sambamba na kuongeza matumizi ya umeme. Ndiyo maana tunasisitiza wananchi wapike kwa umeme na waendeshe vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme,” amesema.
Bw. Twange amemshukuru Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kutembelea banda la TANESCO na kupata fursa ya kujionea miradi na huduma zinazotolewa na shirika hilo, huku akiwashukuru pia wananchi waliotembelea banda hilo na kutoa maoni ambayo yataendelea kusaidia kuboresha huduma za TANESCO nchini.

