Kampuni ya Tanzania Breweries Public Limited Company (TBL) imezindua kampeni ya Cheers to Bars inayolenga kutambua na kusherehekea mchango wa baa za nchini katika kuimarisha mshikamano wa jamii, kukuza biashara ndogo ndogo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa ndani.

Kupitia kampeni hiyo, TBL imesema baa si sehemu za kuburudika pekee, bali ni kitovu cha shughuli za kijamii na kiuchumi ambapo marafiki hukutana, mashabiki wa soka hutazama mechi pamoja na wafanyabiashara mbalimbali hupata fursa za kujiongezea kipato.

Mkurugenzi wa Sheria na Masuala ya Ushirika wa TBL, Neema Temba, amesema kampeni hiyo inalenga kuthamini mchango wa wamiliki wa baa pamoja na wadau wengine wanaonufaika na shughuli zinazofanyika katika maeneo hayo.

“Baa ni sehemu muhimu ya maisha ya kijamii na kiuchumi ya Watanzania. Zinasaidia kujenga maisha ya watu, zinatoa fursa kwa biashara ndogo ndogo na zinatoa nafasi kwa jamii kukutana na kuimarisha mahusiano. Kupitia Cheers to Bars, tunazisherekea baa hizi pamoja na watu wanaoziendesha, huku tukiwahamasisha watumiaji kufurahia vinywaji kwa kuwajibika,” amesema Temba.

Amesema kampeni hiyo pia inaonesha nafasi ya baa wakati wa matukio makubwa ya michezo, hususan soka, ambapo mashabiki wengi hupendelea kutazama mechi katika mazingira yanayowawezesha kushirikiana na wengine.

Katika utekelezaji wa kampeni hiyo, mashabiki walikusanyika katika Baa ya Kitambaa Cheupe jijini Dar es Salaam kushuhudia mechi ya robo fainali kati ya Hispania na Ubelgiji, ambapo walishirikiana kushangilia na kufurahia mchezo huo, hali iliyoonesha namna baa zinavyogeuza matukio ya kimataifa kuwa uzoefu wa pamoja kwa jamii.

TBL imeeleza kuwa wakati wa mechi kubwa, shughuli katika baa huongeza kipato kwa wadau mbalimbali wakiwemo wauzaji wa chakula, wasambazaji wa bidhaa, walinzi, wahudumu na watoa huduma za usafiri, hivyo kuchangia ukuaji wa sekta ya ukarimu na burudani.

Kupitia kampeni ya Cheers to Bars, TBL imeendelea kuhimiza matumizi ya vinywaji kwa kuwajibika, kuunga mkono baa za kienyeji na kuendelea kujenga mazingira salama na yenye furaha kwa jamii, huku ikisisitiza kuwa kumbukumbu nyingi za soka hujengwa si uwanjani pekee bali pia katika baa zinazowaunganisha Watanzania.