Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Abdallah Mwaipaya amezitaka taasisi binafsi, za kifedha na Wadau wa Maendeleo nchini kuaendelea kuwaunga mkono wanufaika wa mafunzo ya ufundi stadi kupitia mradi wa Dumisha Amani uliofadhiliwa na mashirika ya kimataifa ya UNPDF, UNDP, CPP wakishirikiana na GPF Tanzania.

Mwaipaya ametoa wito huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, tarehe 12 Julai, 2026 wakati wa hafla fupi ya ufungaji rasmi wa mafunzo kwa wanufaika wa mradi huo iliyofanyika katika Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Mtwara (chuo cha VETA Mtwara).

“Nitoe wito kwa taasisi binafisi na zakifedha pamoja na wadau wa maendeleo kuendelea kuwaunga mkono vijana hawa kwa kuwapatia mahitaji, vifaa vya kazi, masoko na fursa za ajira ili ujuzi walioupata uweze kuzaa matokeo yaliyokusudiwa,” amesema Mwaipaya.

Sambamba na hilo Mwaipaya amewapongeza wahitimu hao kwa nidhamu na juhudi walizoonesha katika kipindi chote cha mafunzo hata hivyo amewataka vijana hao kwenda kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao na kutumia ujuzi walioupata kuongeza thamani ya mazao na kujiajiri kwa kuanzisha biashara zitakazosaidia kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira na kuimarisha uchumi wa familia na Taifa.

Kwa upande wake Shigeki Komatsubara, Mkurugenzi Mkazi shirika la UNDP-Tanzania amesema awamu ya pili ya Mradi wa Dumisha Amani itaendelea kuongeza fursa za uwekezaji kwa vijana wa Mtwara pamoja na kufanya ukaratabati wa vyumba vya madarasa, ununuzi wa nyenzo muhimu za kujifunzia na kufundishia pamoja na kuanzisha Kituo cha Vijana (Youth Centre) ili vijana waendelee kujifunza na kuwa wabunifu na kuleta maendeleo katika jamii inayowazunguka.Naye Balozi wa Jamhuri ya watu wa China Nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian, amewataka wahitimu hao Kwenda kutumia vyema ujuzi walioupata ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.Aidha Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amewashukuru wafadhili wa mradi huo akisema kuwa ni ishara ya ushirikiano mzuri na endelevu wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na mataifa mengine.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wenzake Mesia Jimmy amesema ujuzi walioupata hautaishia darasani bali watautumia kuanziasha biashara, kujiajiri na kuajiri vijana wengine pamoja nakuendelea kuwa mabalozi wa amani popote watakapokuwa.

Mradi wa Dumisha Amani umetekelezwa katika vyuo 4 vya VETA ambavyo ni Mtwara, Lindi, Songea na Kigoma na kunufaisha vijana 240.