Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya mawasiliano ya Yas imeendelea kuwazawadia wateja wake kupitia kampeni ya Kombe la Dunia ya MiXX Super, ambapo washindi watatu wamekabidhiwa zawadi za shilingi milioni moja kila mmoja kwa kutumia programu ya MiXX Super kufanya malipo ya huduma mbalimbali.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi hizo katika banda la Yas kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Meneja wa Biashara wa Yas Mkoa wa Dar es Salaam, Estony Venant, alisema kampeni hiyo imeendelea kuwagusa Watanzania wengi huku jumla ya washindi 48 wakinufaika hadi sasa.

Alisema kati ya washindi hao, 20 wamejishindia vifaa mbalimbali kutoka kwa mshirika wa Yas, kampuni ya Hisense, huku washindi wengine 28 wakijishindia fedha taslimu za shilingi milioni moja kila mmoja.

Venant alisema kampeni hiyo bado inaendelea na kwamba mshindi wa mwisho atajishindia zawadi kubwa ya shilingi milioni 50, akiwahimiza wananchi kutumia programu ya MiXX Super katika kufanya malipo ya huduma mbalimbali ili kuongeza nafasi ya kushinda.

“MiXX Super ni zaidi ya programu ya malipo; ni jukwaa linalorahisisha huduma za kifedha huku likiwapa watumiaji nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali. Tunawahimiza wananchi kuipakua na kuitumia mara kwa mara,” alisema Venant.

Mmoja wa washindi wa shilingi milioni moja, Thabit Haruna, alisema matumizi ya MiXX Super yamekuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku kwa kuwa yanamwezesha kufanya malipo kwa urahisi bila kulazimika kubeba fedha taslimu nyingi.

Alisema programu hiyo ni salama, rahisi kutumia na imeongeza urahisi katika kulipia huduma mbalimbali, huku akiwashauri Watanzania wengi zaidi kujiunga na kuitumia ili kufurahia huduma zake pamoja na nafasi ya kushinda zawadi zinazotolewa kupitia kampeni hiyo.