Na Happy Lazaro, Arusha .
Vijana nchini wametakiwa kuachana na tabia ya kukaa vijiweni na badala yake kujiunga katika vikundi, kuanzisha miradi yenye tija na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ili kujenga uchumi wao binafsi na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Wazo Mwang’onda, wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Themi, Jiji la Arusha, ambapo alitembelea kikundi cha vijana cha Mclives Limited kilichonufaika na mkopo wa Sh milioni 30 kutoka Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Mwang’onda amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwawezesha vijana kiuchumi, ikiwemo kuelekeza halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo na riba kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Amesema vijana wanapaswa kutumia fursa hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili kuwawezesha vijana wengine kunufaika na kuongeza mchango wao katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“Serikali imeleta fursa hizi ili vijana wajikomboe kiuchumi. Ni muhimu kutumia mikopo hiyo kwa maendeleo, kufanya kazi kwa bidii na kurejesha fedha kwa wakati ili vijana wengine waweze kupata nafasi kama mlivyopata,” amesema.
Ameeleza kuwa kabla ya kupata mkopo huo, wanachama wa Mclives Limited walikuwa wakifanya shughuli ndogo ndogo za kujipatia kipato ikiwemo uuzaji wa uji, lakini baada ya kupata mtaji waliweza kupanua shughuli zao na kuanzisha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zenye kuongeza thamani.
“Kwa sasa kikundi hicho kinamiliki mashine za kusaga nafaka, kutengeneza unga wa lishe, kukamua mafuta ya alizeti, kukausha mazao pamoja na kuzalisha bidhaa mbalimbali za kilimo, hatua ambayo imeongeza ajira na kipato kwa wanakikundi huku ikiwasaidia wakulima kupata soko la uhakika la mazao yao.”amesema .
Aidha, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amesema Serikali imeendelea kupanua fursa za kiuchumi kwa vijana kupitia mpango wa kutenga asilimia 30 ya thamani ya zabuni za taasisi za umma kwa ajili ya makundi maalumu, ikiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Mclives Limited, Hilda Mmari, ameishukuru Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kuwawezesha kupata mkopo wa Sh milioni 30 uliowawezesha kununua mashine nne za uchakataji wa mazao ya kilimo na kuboresha uzalishaji wa bidhaa bora.
Amesema mradi huo umeleta manufaa makubwa kwa kikundi hicho na jamii kwa ujumla kwa kuongeza ajira, kukuza kipato na kuwasaidia wakulima wa soya pamoja na mazao mengine kupata soko la uhakika la malighafi.

