Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete akiteta jambo na Bw. Ban Ki-moon, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN)Rais Mstaafu Dkt. Kikwete akimkabidhi Bw. Ban Ki-moon Kitabu kinachoonesha kazi za Taasisi ya GPE katika nchi zaidi ya 90 duniani kote.

 Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete akimkabidhi Bi. Kim Jina, Makamu wa Pili wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kitabu kinachoonesha kazi za Taasisi ya GPE baada ya mazungumzo yaoRais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na Makamu wa Pili wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini, Bi. Kim Jina. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bw. Noel Kaganda pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini na Taasisi ya GPE.

Picha ya pamoja baada ya mazungumzo: Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Pili wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini, Kim Jina, kulia kwake ni Bw. Pádraig Power, Afisa Mkuu wa Fedha (CFO) wa GPE, Bi. Yukiko Matsuyoshi, Mtaalamu wa Elimu na Msimamizi wa Mahusiano wa GPE, Bw. Noel Kaganda, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini na Profesa Utak Chung, Mshauri Mkuu wa GPE nchini Korea Kusini.Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete baada ya mazungumzo na Bw. Chang Wook-jin, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kusini anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiweka alama ya upendo ya Korea Kusini kwa vidole na Mbunge Bi. Kyung-sook Kang baada ya mazungumzo yao.

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wa GPE aliombatana nao katika picha ya pamoja baada ya mazungumzo na Mbunge Bi. Jae Jung Lee. Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akipozi katika picha na Mbunge wa Korea Kusini Bw. Geon Kim (kulia) na Bw. Youngkey Hwang, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Chorogwoosan (ChildFund Korea) ya Korea Kusini ambayo inasimamia ufadhili wa GPE katika miradi mbalimbali (grants agent)

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akitoa mhadhara kuhusu umuhimu wa elimu ya awali na ya msingi katika Chuo Kikuu cha Seoul National University ikiwa ni sehemu za ziara yake nchini Korea Kusini.

Bi. Su Jin Moon, Mwanafunzi wa Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Seoul National University akiuliza swali katika mhadhara uliotolewa na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Chuo hicho

………..

Rais Mstaafu Dkt. Mrisho Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Ban Ki-moon, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu kukuza elimu ya awali na msingi duniani kupitia Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education – GPE).

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Seoul, Korea Kusini ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi ya Dkt. Kikwete anayoifanya nchini humo kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya GPE kukutana na Viongozi wa Serikali ya Korea pamoja na mashirika wadau wa GPE kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya GPE na wadau wa nchi za mashariki ya mbali, hususan Korea Kusini na Japan.

Katika mazungumzo yake na Ban Ki-moon, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Taasisi za The Ban Ki-moon Foundation yenye makao yake makuu Vienna nchini Austria, na Ban Ki-moon Foundation for a Better Future yenye makao yake makuu Seoul, Korea Kusini, Rais Mstaafu Dkt. Kikwete amempongeza Katibu Mkuu huyo Mstaafu wa UN kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kupitia Taasisi zake ya kuhamasisha ufikiwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan Lengo Namba 4 linalohusu Elimu Bora kwa Wote, Lengo Namba 13 linalohusu Kuchukua Hatua dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi, na Lengo Namba 17 linalohusu Ushirikiano wa Kimataifa kati ya Serikali, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia katika kutimiza malengo ya SDG.

Dkt. Kikwete alitumia fursa hiyo pia kumshukuru Bw. Ban Ki-moon kwa msaada wake anaoutoa kwa Taasisi ya GPE uliowezesha kuimarika kwa mahusiano kati ya Taasisi hiyo ya GPE na Serikali ya Korea Kusini. Kwa mujibu wa taarifa inayopatikana kwenye tovuti ya GPE, Korea Kusini ni moja ya nchi na mashirika wafadhili 33 (donor countries organisation) wa GPE ambayo tangu mwaka 2015 imeshachangia jumla ya Dola za Kimarekeni milioni 20 kwa Taasisi hiyo.

Kwa upande wake Bw. Ban Ki-moon amemhakikishia Dkt. Kikwete kuwa ataendelea Taasisi zake zitaendelea kufanya kazi kwa karibu na Taasisi ya GPE, Serikali ya Korea na mashirika mengine ya kimataifa katika kukuza elimu duniani, hususan kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu. Katika mazungumzo yao, Bw. Ban Ki-moon alisisitiza umuhimu wa elimu katika kufungua fursa za kila mtoto duniani, huku akitoa mfano wa namna elimu bora imekuwa ufunguo katika maisha yake akieleza namna kijiji chake kiliteketezwa na moto katika Vita ya Korea ya mwaka 1950 – 1953 ambapo walilazimika kusomea chini ya mti, na kwamba ufadhili wa chakula na elimu uliotolewa na Umoja wa Mataifa ndiyo uliokoa maisha yake na kumuandaa kuja kuwa kiongozi mkubwa duniani.

Kwa upande mwingine, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete alikutana na Viongozi mbalimbali wa Serikali ya Korea Kusini wakiwemo Makamu wa Pili wa Waziri wa Mambo ya Nje, Kim Jina, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa, Chang Wook-jin pamoja na Wabunge Jae Jung Lee, Kyung-sook Kang na Geong Kim wanaohusika na masuala ya elimu na ushirikiano wa maendeleo ya kimataifa ya Korea Kusini.

Dkt. Kikwete ametumia fursa ya kukutana na Viongozi hao kuishukuru Serikali ya Korea Kusini kwa kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Taasisi ya GPE, si tu kwa kutoa ufadhili wa kifedha, bali pia kwa kutoa uzoefu wake katika kuendeleza sekta ya elimu kwa nchi nyingine duniani, huku nchi hiyo ikisifika kwa viwango vya juu vya elimu ya hisabati, sayansi na ubunifu. Kwa upande wao, pamoja na mambo mengine, Viongozi hao walieleza nia ya Serikali ya Korea kudumisha ushirikiano huo na kwamba inanuia kutangaza kuongeza kiwango cha fedha inachotoa kufadhili GPE katika Mkutano wa Ahadi (Replenishment Summit) utakaofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), New York, tarehe 23 Septemba, 2026.

Taasisi ya GPE imelenga kutumia Mkutano huo wa New York, Marekani kuzindua Kampeni ijulikanayo kama GPE 2030 ambapo jumla Dola za Marekani bilioni 15 zinatarajiwa kukusanywa kati ya mwaka 2026 – 2030 ili kugharamia elimu ya awali na msingi kwa watoto takribani milioni 750 katika nchi zaidi ya 90 kote duniani ikiwemo Tanzania.

Tanzania ni moja ya nchi wanufaika wa fedha zinazotolewa na Taasisi ya GPE ambapo hadi sasa imeshapokea zaidi ya Dola za Marekani milioni 207.3 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini. Inatarajiwa kuwa kiasi hicho cha fedha kinachotolewa kwa Tanzania kitaogezeka kupitia mpango wa GPE wa kuziongezea fedha za ufadhili nchi zinazofanya vizuri katika kusimamia sekta ya elimu ya miradi inayotekelezwa kwa ubia kati ya Serikali na Taasisi ya GPE.

Balozi mpya wa Tanzania nchini Korea Kusini Noel Kaganda alishiriki katika baadhi ya mikutano hiyo iliyofanywa na Rais Mstaafu Dkt. Kikwete na Viongozi hao mbalimbali wa Korea Kusini.

Aidha, kwa nafasi yake ya Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwa kutambua mchango na nafasi yake katika kukuza na kuendeleza sekta ya elimu nchini Tanzania na duniani kote, Chuo Kikuu cha Seoul National University kilimwalika Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kutoa mhadhara wa wazi katika Chuo hiko.