Mawaziri wanaosimamia sekta za Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameazimia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu ya barabara, reli, usafiri wa anga na viwanja vya ndege, usafiri wa majini pamoja na sekta ndogo ya mawasiliano ili kuimarisha mtangamano wa kikanda, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.
Azimio hilo limefikiwa katika Mkutano wa 20 wa Baraza la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (TCM) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Julai 10, 2026, katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.
Mkutano huo umejadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi ya mkutano uliopita wa TCM, hususan kuhusu miradi na programu za kikanda katika sekta za barabara, reli, usafiri wa anga na viwanja vya ndege, usafiri wa majini pamoja na mawasiliano.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey M. Kasekenya (Mb), alisema kuwa miundombinu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na nguzo muhimu katika kuimarisha mtangamano wa nchi wanachama, kuvutia uwekezaji, kuongeza fursa za ajira na kuboresha mazingira ya biashara.
“Sote tunatambua kuwa sekta za barabara, reli, usafiri wa anga na mawasiliano ni msingi wa maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi wetu. Aidha, sekta hizi zina mchango mkubwa katika kuongeza ushindani wa nchi zetu na Jumuiya, katika soko la kikanda na kimataifa,” alisema Mhe. Mhandisi Kasekenya.
Miongoni mwa miradi ya kimkakati iliyopewa kipaumbele ni ujenzi wa barabara za Masaka–Mutukula/Mutukula–Kyaka, Bugene–Kasulo–Kumunazi, Malindi–Mombasa–Lunga Lunga/Tanga–Bagamoyo, Nyakanazi–Kasulu–Manyovu/Rumonge–Bujumbura, Arusha–Holili–Mwatate, Lusahunga–Rusumo/Kayonza–Kigali, pamoja na utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa Vituo vya Huduma Pamoja Mipakani (One Stop Border Posts – OSBPs).
Vilevile, Mawaziri wameielekeza Sekretarieti ya EAC kuharakisha ukamilishaji wa programu mbalimbali ambazo utekelezaji wake unaendelea. Programu hizo ni pamoja na Mkakati wa Usalama Barabarani wa Afrika Mashariki, mpango wa kuoanisha tozo za matumizi ya barabara kwa magari ya kigeni katika nchi wanachama wa EAC, mapitio ya mfumo wa udhibiti wa uzito wa magari wa EAC, pamoja na programu ya pamoja ya utafutaji na uokoaji katika anga na majini.
Mbali na hayo, mkutano umekubaliana kuwa nchi wanachama na Sekretarieti ya EAC ziendelee kutafuta rasilimali fedha ili kukamilisha miradi iliyokwama kutokana na changamoto ya ukosefu wa fedha. Taarifa iliyowasilishwa katika mkutano imeonesha kuwa jumla ya miradi 22 kati ya 66 bado inakabiliwa na changamoto za ufadhili.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey M. Kasekenya (Mb), ukiambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Millya (Mb), Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile (Mb), Makatibu Wakuu wa sekta husika pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.

