NA DENIS MLOWE, IRINGA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ameipongeza BRAC Maendeleo Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha wanawake, wasichana na makundi maalum kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoboresha maisha ya wananchi.
Dkt. Gwajima amesema hayo alipofanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na BRAC Maendeleo mkoani Iringa, ambapo alieleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kufanikisha malengo ya taifa ya maendeleo.
Alisema miradi inayotekelezwa na BRAC inalenga kuwawezesha wasichana na wanawake kiuchumi pamoja na kuboresha malezi na makuzi ya watoto, jambo linaloendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga jamii yenye watu bora na wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
“Nchi ni kubwa na wananchi ni wengi, Serikali peke yake haiwezi kufanya kila kitu. Ushirikiano na wadau wa maendeleo kama BRAC ni muhimu katika kufikia wananchi wengi zaidi,” alisema Dkt. Gwajima.
Alieleza kuwa mradi wa BRAC unaowalenga wasichana na wanawake wenye umri wa miaka 12 hadi 35 unatekelezwa katika mikoa nane ambayo ni Iringa, Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro, Tabora, Mbeya, Tanga na Mwanza, ukihusisha halmashauri 39 na unatarajiwa kuwafikia wanufaika zaidi ya 140,361.
Aidha alisema mradi huo ulioanza mwaka 2023 unatarajiwa kutekelezwa hadi mwaka 2033 kwa gharama ya dola za Marekani milioni 23, fedha ambazo alisema zitatoa mchango mkubwa katika kuwawezesha wanawake na wasichana pamoja na kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Iringa, Saida Mgeni, alisema Serikali imeendelea kuimarisha huduma za maendeleo ya jamii kwa kuajiri maafisa maendeleo ya jamii 191, huku kata 106 kati ya zote za mkoa huo zikiwa tayari zina maafisa hao.
Alisema katika mwaka wa fedha unaomalizika, mkoa umefanikiwa kuhuisha majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi na mabaraza ya watoto katika kata zote 106, hatua inayosaidia kusogeza huduma karibu na wananchi.
Saida alisema Mkoa wa Iringa una mashirika yasiyo ya kiserikali 180 yanayotekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo, huku BRAC ikiwa miongoni mwa mashirika yaliyofanya kazi kwa karibu na Serikali na jamii tangu kuanza kwa shughuli zake mwaka 2023.
Alisema kuwa BRAC imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza programu zinazowafikia wananchi hadi ngazi ya vijiji, ikishirikiana na maafisa maendeleo ya jamii, viongozi wa vijiji na wananchi katika utekelezaji wa miradi yake.
Naye Naibu Mkurugenzi wa BRAC Maendeleo Tanzania, Nasikiwa Duke Mwalisu, alisema kupitia Mradi wa kuwezesha vijana wa kike (Accelerating Impact for Young Women – AIM), taasisi hiyo inalenga kuwafikia wasichana na wanawake 725,252 wenye umri wa miaka 12 hadi 35 katika kipindi cha miaka 10.
Alisema asilimia 35 ya wanufaika watapata msaada wa kifedha utakaowasaidia kuendelea au kurejea shuleni, huku asilimia 65 wakipatiwa mafunzo ya ujuzi, vifaa na mtaji wa kuwawezesha kuanzisha shughuli za kujiongezea kipato.
Mbali na hilo, alisema BRAC itashirikiana na shule 400 kuboresha mazingira ya kujifunzia, kuanzisha vikundi vya kijamii zaidi ya 13,040 na vituo 300 vya malezi ya awali ya watoto, pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu zaidi ya 500 wa vituo hivyo.
Kwa Mkoa wa Iringa pekee, Mwalisu alisema tangu kuanza kwa mradi mwaka 2023, BRAC imewafikia washiriki 17,040, imeanzisha vituo 10 vya malezi ya awali ya watoto vilivyohudumia watoto 165, pamoja na kuendelea kuwezesha vikundi vya kijamii vinavyojihusisha na kilimo, ufugaji, biashara ndogo ndogo na shughuli nyingine za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Iringa (NaCoNGO), Fidelis Emilio Filipatari, alisema ujio wa Waziri huyo ni ishara ya kutambua mchango mkubwa wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuleta maendeleo nchini.
Alisema mkoani Iringa kuna mashirika 431 yaliyosajiliwa ambayo yanatekeleza afua mbalimbali zikiwemo za watoto, maji, elimu, afya, uchumi, ujasiriamali na maendeleo ya jamii, huku yakisaidia kufikisha huduma katika maeneo ambayo Serikali haijafikia kwa kiwango kinachohitajika.
Filipatari alisema mashirika hayo hufanya kazi kwa kushirikiana na Serikali katika ngazi ya vijiji kwa kutoa elimu, kuunda vikundi vya kiuchumi, kuwawezesha wananchi kuanzisha biashara kupitia mitaji, pamoja na kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii.
Alisema NaCoNGO inaendelea kuhimiza mashirika kuhakikisha miradi yao inakuwa endelevu badala ya kutegemea ufadhili pekee, ili hata wafadhili wanapoondoka, wananchi waendelee kunufaika na miradi iliyoanzishwa.
Aidha, alitoa wito kwa Serikali kuendelea kushirikiana kwa karibu na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaendelezwa baada ya kipindi cha ufadhili kumalizika, badala ya kuachwa kuwa magofu au kusimama kabisa.
Filipatari pia alitoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kupanga vizuri maeneo ya utekelezaji wa miradi yao ili kuepusha mashirika mengi kufanya shughuli zinazofanana katika eneo moja, huku maeneo mengine yakikosa huduma muhimu.
Alisema hatua hiyo itasaidia kupanua wigo wa huduma, kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha za wafadhili, jambo ambalo pia huongeza imani ya wafadhili kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo nchini.