Na. Veronica Mwafisi-Sikonge
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameendelea na ziara yake ya kikazi ya siku tatu aliyoianza jana mkoani Tabora ambapo leo tarehe 9 Julai, 2026 ameingia wilayani Sikonge na kuwasisitiza Viongozi na Watendaji kuwaambia wananchi mazuri yaliyofanywa na Serikali.
Akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, mara tu baada ya kufika katika Wilaya hiyo, Mhe. Kikwete amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mambo mengi makubwa katika sekta mbalimbali lakini wananchi hawajui hivyo, ni wakati sasa Viongozi na Watendaji kutoka kuwaambia wananchi badala ya kusubiri viongozi kutoka maeneo mengine kuja kuzungumza.
“Viongozi wetu watoke kuzungumza na wananchi na kusikiliza changamoto, wananchi walalamike kwa changamoto nyingine labda ya kutokujitosheleza kwa huduma lakini sio kwa kukosa taarifa, ni wajbu wetu kuwaambia,” amesisitiza.
Ametoa wito kwa Viongozi hao kushughulikia changamoto za wananchi zilizo ndani ya uwezo wao na kuwaambia ukweli sababu zinazokwamisha baadhi ya changamoto kutoshughulikiwa kwa wakati ili kuepusha migogoro, Aidha ameongeza kuwa changamoto zilizo nje ya uwezo wao wasikae nazo kimya bali washirikishe ili kuona namna ya kuzitatua.
Amesema majukumu wanayoyatekeleza ni kwa niaba ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan yanayozingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025 lengo likiwa ni kuhakikisha changamoto za wananchi zinafanyiwa kazi ili kuepusha malalamiko na kulinda amani ya nchi.

