Na. Veronica Mwafisi-Manispaa ya Tabora

Tarehe 09 Julai, 2026

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka Viongozi mkoani Tabora kuzingatia vigezo vya kuwapata walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mhe. Kikwete amesema moja ya jambo kubwa ambalo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akilisisitiza ni kusaidia Watanzania walio wanyonge. “TASAF awamu zilizopita illishia mwaka jana mwezi wa 9 lakini kwa upendo wake amepambana kuhakikisha fedha zinapatikana ili kusaidia Watanzania hao kuepukana na umaskini,” Mhe. Kikwete ameongeza.

Akizungumza na Wananchi katika Manispaa ya Tabora tarehe 9 Julai, 2026, baada ya kuhitimisha ziara yake kwa siku ya leo aliyoifanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Halmashauri ya Wilaya ya Tabora na Manispaa ya Tabora ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Mhe. Ridhiwani amesema sio sawa fedha hizo zikatumika kinyume kwa kuwaingiza kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini watu wasiostahili. “Niwaombe mliopewa dhamana ya kusimamia zoezi hili kutenda haki kwa kuwaweka walengwa stahiki,” Mhe. Kikwete ameongeza.

Amesema kuna baadhi ya maeneo yalilalamikiwa kwa kufanya mambo ya ajabu na kutowatendea haki walengwa katika fedha walizokuwa wakipewa, niwaombe sana, tunapoanza mpango unaokuja, nisingependa yale mapungufu yaliyojitokeza kipindi cha nyuma yajirudie.

Ametoa wito kwa Wananchi kushiriki katika mikutano ya kutambua walengwa ili wapatikane watu sahihi. “Wananchi nanyi kwa kuwa mnashiriki katika mikutano ya kuibua walengwa, mkisomewa majina ya walengwa kama kuna ambao wameachwa mseme ili waongezwe na kama wamewekwa wasiostahili pia mseme ili watolewe kwani mkikaa kimya ndio matokeo yake wanaingizwa wasiostahili na baadae kuleta malalamiko.” ameongeza