Na. Veronica Mwafisi-Sikonge na Tabora
Tarehe 09 Julai, 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameisihi Kamati ya Miradi ya Maendeleo mkoani Tabora kusimamia kwa umakini miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali mkoani humo ili iendane na thamani halisi ya fedha.
Mhe. Kikwete amesema hayo kwa nyakati tofauti leo tarehe 9 Julai, 2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Halmashauri ya Wilaya ya Tabora na Manispaa ya Tabora wakati akikagua na kuweka jiwe la msingi na kuzindua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Tabora.
Amesema katika kuhakikisha nchi inakuwa na maendeleo kwenye sekta zote, Serikali itaendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo, hivyo ni jukumu la wasimamizi kusimamia kwa ufasaha ili miradi hiyo itekelezwe kikamilifu kulingana na fedha inayotolewa.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika kituo cha afya cha Igigwe, Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Mhe. Kikwete amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kusema Serikali inahitaji eneo kubwa ili kujenga majengo mengi zaidi kwa lengo la kuwa na huduma mbalimbali za afya.
“Kituo hiki cha afya ni kwa ajili ya wagonjwa wa nje, hivyo tunahitaji eneo kubwa zaidi ili tuweke majengo mengi kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi,” ameongeza.
Akizungumza katika hatua nyingine mara baada ya kuzindua majengo ya Shule ya Msingi Kigamboni katika Halmashauri ya Wilaya ya Tabora, Mhe. Kikwete amesema Sera ya Elimu ni kuhakikisha vijana wanapata elimu jirani badala ya kutembea umbali mrefu.
Amesema lengo la Serikali ni kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kutafuta elimu na ndio maana inajenga shule jirani ili wapate muda mrefu wa kusoma badala ya kutumia muda huo kutembea.
Aidha, ameongeza kuwa wingi wa majengo unasaidia kupunguza idadi ya wanafunzi kurundikana kwenye darasa moja na kuwarahisishia Walimu kufundisha na wanafunzi kupata uelewa.
“Zamani wakati sisi tunasoma, darasa moja lilikuwa na wanafunzi wengi kwasababu madarasa yalikuwa machache, lakini sasa hivi madarasa mengi hivyo wanafunzi katika darasa moja hawazidi 45, aidha Walimu wanapata muda wa kuwa na wanafunzi karibu wanaoweza kuwamudu, wanafunzi sasa hivi mtake wenyewe kufeli,” ameongeza.
Amesema akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana wa masuala ya Utumishi, atahakikisha anasimamia zoezi la kupatikana kwa Walimu wa kutosha ili wanafunzi wapate elimu bora.
“Majengo yamejengwa, ni mazuri, hata sehemu nyingine mjini hakuna majengo kama haya, hivyo wanafunzi muhakikishe mnafanya vizuri katika masomo yenu, tutaleta Walimu ili watoto wapate elimu bora huku akisisitiza utunzaji wa majengo hayo ili yadumu muda mrefu.
Suala la usimamizi wa miradi ya maendeleo amelisisitiza tena wakati akikagua na kuzindua kituo cha afya cha Maili Tano katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
“Hongereni kwa kazi nzuri, kikubwa niwasisitize usimamizi katika miradi hii kama nilivyosema hapo awali, ili thamani ya fedha ionekane,” ameongeza.
Mhe. Ridhiwani amehitimisha ziara yake kwa siku ya leo kwa kuzungumza na Wananchi Manispaa ya Tabora ambapo alipata fursa pia ya kusikiliza changamoto zao kwa lengo la kuzifanyia kazi.

