Na Mwandishi Wetu

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ujenzi na matengenezo ya barabara nchini kupitia matumizi ya teknolojia bunifu, usimamizi madhubuti wa ubora wa miundombinu pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika matengenezo ya barabara.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Nyamagarura Masatu Ndango alisema mkoa huo unasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 5,057.7, ambapo asilimia 12.6 ni barabara za lami, asilimia 33.3 ni za changarawe na asilimia 54 ni za udongo.

Alisema mbali na matengenezo ya kawaida, TARURA inaendelea kutekeleza Mradi wa Dar es Salaam Metropolitan Development Project (DMDP II), unaohusisha ujenzi wa kilomita 191 za barabara za lami katika wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam, zikiwa na mifereji ya maji ya mvua, taa za barabarani pamoja na njia za waenda kwa miguu.

Aidha alisema TARURA inatekeleza mradi mkubwa wa kuboresha Bonde la Mto Msimbazi unaojumuisha ujenzi wa daraja la mita 390, uimarishaji wa kingo za mto pamoja na usafishaji wa mkondo wa mto hadi eneo la Mikoko. Pia wakala unaendelea na matengenezo ya sehemu korofi, madaraja madogo na vivuko ili kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri kutoka TARURA Makao Makuu, Fares Ngereja, alisema wakala huo unaosimamia jumla ya kilomita 144,149.18 za barabara nchini umeamua kutumia teknolojia mpya kutokana na changamoto za fedha na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema kwa sasa TARURA imeanza majaribio ya ujenzi wa barabara kwa kutumia kemikali maalumu za Polymer na EcoZyme katika maeneo mbalimbali ikiwemo Chamwino, Rufiji, Simiyu na Njombe, huku ubora wake ukiendelea kufanyiwa tathmini na TANROADS kabla ya kuanza kutumika kwa kiwango kikubwa.

Ngereja alisema matumizi ya teknolojia ya mawe katika ujenzi wa madaraja yameleta mafanikio makubwa ambapo zaidi ya madaraja 515 yamejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 43, tofauti na zaidi ya bilioni 153 ambazo zingehitajika kama ingetumika teknolojia ya zege na nondo pekee.

Naye Ofisa kutoka Kitengo cha Utafiti na Udhibiti Ubora TARURA Makao Makuu, Jacob Manguye, alisema maabara za TARURA zina jukumu la kuhakikisha vifaa vya ujenzi na kazi zote za barabara zinakidhi viwango vinavyotakiwa kabla, wakati na baada ya ujenzi.

Alisema TARURA ina maabara Makao Makuu Dodoma pamoja na maabara nyingine katika mikoa 14 nchini ambazo hufanya uchunguzi wa vifaa vya ujenzi na ukaguzi wa miradi ili kuhakikisha miundombinu inayojengwa inadumu kwa muda mrefu.

Manguye aliongeza kuwa TARURA imeanza kutumia mtambo wa kisasa wa Geotechnical unaosaidia kufanya uchunguzi wa udongo kabla ya ujenzi wa madaraja makubwa, majengo na miundombinu mingine, huku akiwakaribisha wadau wa sekta ya ujenzi kutumia huduma za maabara hizo.

Kwa upande mwingine, Mratibu wa Mpango wa Community-based Routine Maintenance (CbRM), Mhandisi Richard Misa, alisema mpango huo unaotekelezwa chini ya Mradi wa RISE unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unalenga kuboresha zaidi ya kilomita 15,000 za barabara pamoja na kuzalisha ajira kupitia vikundi vya wananchi.

Alisema katika mwaka wa fedha 2025/26 tayari vikundi 302 vimenufaika kwa kufanya matengenezo ya kilomita 1,500 za barabara, huku mwaka 2026/27 mpango huo ukitarajiwa kupanuliwa katika mikoa 25, wilaya 70 na halmashauri 104, ambapo zaidi ya kilomita 7,000 zitaboreshwa na zaidi ya vikundi 1,400 vitapata ajira.

Misa alisema mpango huo unalenga kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote kupitia shughuli za kusafisha mifereji, makalavati, madaraja na kuondoa vikwazo mbalimbali, sambamba na kuongeza kipato kwa wananchi wanaoishi jirani na barabara hizo kupitia ajira za matengenezo.

TARURA imeeleza kuwa ubunifu unaotumika katika ujenzi wa barabara na madaraja, pamoja na usimamizi wa ubora na ushirikishwaji wa wananchi, ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha miundombinu na kuongeza huduma za usafiri nchini.