Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imetunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kufanikisha utafiti kuhusu maboresho ya kisasa ya mnyororo wa thamani wa kilimo uliofanywa na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Maendeleo ya Canada (IDRC-CRDI) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Tuzo hiyo imekabidhiwa leo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu, na Meneja wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Bodi hiyo, Bw. Elfaraja Kintingu.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Bw. Bangu amesema heshima hiyo ni uthibitisho wa nafasi muhimu ya WRRB katika kuimarisha sekta ya kilimo kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, ambao umeendelea kuongeza ufanisi wa biashara ya mazao, uwazi wa masoko na ushindani wa bei katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema WRRB itaendelea kushirikiana na taasisi za utafiti na wadau mbalimbali katika kuendeleza ubunifu na maboresho yanayochochea maendeleo ya mnyororo wa thamani wa kilimo kwa manufaa ya wakulima na uchumi wa Taifa.

Awali, akielezea kuhusu tuzo hiyo, Bw. Kintingu amesema imetolewa kwa kutambua ushirikiano na mchango wa WRRB katika kufanikisha utafiti huo, ambapo watafiti walitembelea ghala mbalimbali nchini ili kujionea utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na mchango wake katika kuimarisha biashara ya mazao, kuongeza uwazi wa masoko na kuboresha mnyororo wa thamani wa kilimo.