Mkuu wa mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla akikabithi vitimwendo hivyo kwa wahitaji hao jijini Arusha .
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .MKUU wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla amepokea Vitimwendo 60 vyenye thamani ya Shilingi Milioni 65 kutoka kwa Taasisi ya Kimarekani ya Wheelchair Foundation kwa lengo la kusaidia watu wenye Ulemavu Mkoa wa Arusha.
Aidha Makalla ametoa pongezi kwa Chem Chem Association linalojishughulisha na masuala ya utalii na uhifadhi kwa kuguswa na mahitaji ya wenye ulemavu. kwa kitendo cha kuiunganisha Taasisi hiyo na wenye uhitaji Nchini jambo ambalo amesema linapaswa kuigwa na taasisi zingine kwani bila wao msaada huo usingefika hapa leo.
Akikabithi viti hivyo kwa walengwa hao Makalla amemshukuru Rais wa Taasisi ya Wheelchair Bw. David Behring kwa msaada huo pamoja na kuamua kusafiri kutoka Marekani kuja kukabidhi viti hivyo, akiwakaribisha na kuwahakikishia usalama katika kipindi chote watakachokuwepo Mkoani hapa, ikiwemo katika safari yao ya kutembelea Vivutio vya Utalii vilivyopo Mkoani Arusha.
“Nimeongea na uongozi wa Wheelchair Foundation wanasema wanaipenda Tanzania, Watanzania ni wakarimu, Watanzania wanapenda watu na Tanzania ni Nchi ya amani. Jambo hilo limenifurahisha sana kama Mwenyekiti wa Kamati ya usalama na nimewahakikishia Tanzania itaendelea kuwa salama na hasa kulingana na takwimu za Marekani kuchangia kwa idadi kubwa ya watalii wanaokuja Tanzania.”amesema Makalla.
Kwa upande wake Rais wa Wheelchair Foundation yenye Makao yake makuu Danville, California, Bw.Behring amesema kama familia wamekuwa wakitoa misaada hiyo kwa wenye ulemavu ili kuwapa uhuru na heshima wanayostahili, akisema viti hivyo vitawasaidia kutoka eneo moja kwenda lingine na kuwaruhusu kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi ikiwemo fursa ya watoto kupata elimu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chemchem Association ,Clever Zulu akizungumza kwenye hafla hiyo amesema kuwa ,wamefarijika sana kwa namna taasisi hiyo imeweza kutoa msaada huo kwa wahitaji hao mkoa wa Arusha kwani kitendo hicho no kikubea sana kwa jamii hususani wenye uhitaji.
Zulu amesema kuwa,kitendo cha kuwasaidia wenye uhitaji hao kwa kukabithi vitimwendo hivyo kumeleta faraja kubwa sana kwa walengwa kwani walikuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi sana kutokana na ukosefu wa vitimwendo hivyo .
“Kwa kweli tunamshukuru Bw.Behring kwa msaada huo,na tunamwombea heri na mafanikio zaidi ili waweze kuwasaidia wenye uhitaji zaidi na wakisisitiza kuendelea kushirikiana ili kusaidia wengi zaidi wenye mahitaji muhimu.”amesema Zulu.
Miongoni mwa wanufaika wa viti mwendo, Farida Mwinyi ( 34 )kutoka Njiro amesema msaada huo utabadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa kutokana na changamoto za utembeaji alizokuwa akikabiliana nazo nyumbani.
Amesema mazingira ya nyumbani kwake hayakuwa rafiki kwa mtu mwenye ulemavu, kwani wakati wa kwenda msalani au kutoka sebuleni kuelekea chumbani alilazimika kubebwa na mtu mwingine.
Kwa upande wake, mnufaika mwingine, Sebastian Gabriel, ( 50 )mkazi wa Kisongo, Arusha, amesema kabla ya kupata kiti mwendo alikuwa akitumia magongo ambayo yalikuwa yakimsababishia maumivu na kumfanya ashindwe kutembea kwa urahisi.
Amesema kupokea kiti mwendo kutamwezesha kusafiri kwa urahisi kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kumrahisishia shughuli zake za kila siku.
Aidha, amesema kuwa anajishughulisha na kilimo, hivyo kiti hicho kitamsaidia kufika shambani na kuendelea na shughuli zake za kujipatia kipato bila vikwazo vikubwa vya usafiri.

