Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uwasilishaji wa Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar tarehe 09 Julai, 2026.
……….
Na Mwandishi wetu, Zanzibar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaonya watu wanaojitambulisha kuwa wanaharakati lakini wakijihusisha na vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa nchi, akisema Serikali haitavumilia vitendo vyenye sura ya ugaidi kwa kisingizio cha kutetea ajenda za kisiasa au kiitikadi.
Akizungumza leo Julai 9, 2026 Ikulu Zanzibar katika hafla ya utiaji saini wa maridhiano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo, Rais Samia alisema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia jina la uanaharakati kuficha vitendo vya uchochezi, uharibifu wa mali na miundombinu pamoja na kuvuruga utulivu wa nchi.
“Nataka nitumie fursa hii kuwaonya wale wote wanaojiita wanaharakati, lakini kiuhalisia matendo yao yameathiri amani kwa kujihusisha na vitendo vya vurugu, uharibifu wa mali na miundombinu vinavyolenga kushinikiza Serikali kwa ajili ya kutimiza ajenda zao za kisiasa au kiitikadi,” alisema Rais Samia.
Alisema pia wapo wanaovaa sura ya uzalendo, lakini kwa undani wanasukumwa na maslahi binafsi yanayolenga kulichafua taifa, akisisitiza kuwa uzalendo wa kweli haujengwi kwa kuharibu nchi.
“Mtu anayependa nchi yake kwa kweli hawezi kuharibu amani yake. Sisi tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa mazungumzo, hatukuharibu nchi yetu wala kufanya vurugu,” alisema.
Rais Samia aliwataka Watanzania kuendelea kushikamana na kulinda amani, akieleza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana katika mazingira ya machafuko na migogoro ya kisiasa.
Aidha, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kusimama imara katika kulinda usalama wa raia na mali zao, huku akionya kuwa Tanzania haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kigaidi au kuhatarisha usalama wa taifa.
“Niwahakikishie Watanzania kuwa Serikali yenu inasimama imara katika ulinzi wa raia wake na mali zao. Nawaonya kwa mara nyingine wale wote wanaojishughulisha na vitendo hivyo kwamba taifa lolote duniani hutumia nguvu za kisheria kulinda raia wake na heshima yake. Nasi Tanzania hatutasita kufanya hivyo,” alisema.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na kwamba maridhiano yaliyofikiwa kati ya CCM na ACT Wazalendo yanapaswa kuwa mfano wa kutatua tofauti kwa njia ya mazungumzo badala ya migogoro.
Alimalizia kwa kuwataka viongozi na wananchi kuendelea kulinda umoja wa taifa, akisema, “Amani ni mtaji, maridhiano ni daraja, na wananchi ndiyo sababu ya uongozi wetu. Tuendelee kushirikiana na kulinda amani ya Tanzania.”
