Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST) umetunukiwa tuzo ya kimataifa na kutambuliwa kuwa miongoni mwa mifumo 20 bora ya Serikali Mtandao duniani, katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Kimataifa za ‘World Summit on the Information Society (WSIS) Prizes 2026’, iliyofanyika Julai 8, 2026, jijini Geneva, Uswisi.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba, na Mratibu Mkuu wa Tuzo za WSIS, Bi. Gitanjali Sah, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU).

Kwa mujibu wa ITU, tuzo hiyo ilitolewa katika kategoria ya Serikali Mtandao (e-Government), iliyoshirikisha zaidi ya mifumo 1,500 kutoka nchi 122 duniani, ambapo mifumo ilitathminiwa kwa mchango wake katika kukuza uchumi shirikishi, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu kupitia matumizi ya teknolojia.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Simba, alisema mafanikio hayo yametokana na Uongozi na Maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuhimiza matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma za umma kwa kuhakikisha mifumo inasomana ili kutoa urahisi wa huduma.

“Tuzo hii ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na maono yake ya kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za umma,” alisema Bw. Simba.

Aidha, aliwashukuru wadau wa sekta ya Ununuzi wa Umma kwa kuupokea na kuutumia kwa ufanisi Mfumo wa NeST, akibainisha kuwa maoni na ushirikiano wao vimechangia kuendelea kuuboresha mfumo huo, ambao umejengwa na wataalamu wa Kitanzania.

Kwa sasa, michakato yote ya ununuzi wa umma nchini Tanzania inafanyika kupitia Mfumo wa NeST, na kufanya ununuzi nje ya mfumo huo ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023.