Mbunge wa Jimbo la Kilindi, Mhe. Salehe Mbwana Mhando, ameendelea na utaratibu wake wa kuwafikia wananchi kwa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wakazi wa Kata ya Mkindi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusikiliza changamoto zao na kupokea maoni kuhusu maendeleo ya jimbo hilo.
Katika mkutano huo, wananchi walipata fursa ya kueleza kero mbalimbali zinazowakabili katika sekta za huduma za jamii, miundombinu na maendeleo ya kiuchumi, huku Mbunge huyo akiahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na Serikali pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali.
Mhe. Mhando alisema kuwa mawasiliano ya karibu kati ya viongozi na wananchi ni msingi wa kupata suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya jamii.
Wananchi wa kata ya Mkindi walimshukuru mbunge wao kwa kuendelea kutenga muda wa kukutana nao mara kwa mara, wakisema utaratibu huo unaimarisha ushirikiano, uwazi na kuleta matumaini ya kupatikana kwa ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

