
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na Makamu wa Rais Mwandamizi wa Kampuni ya Alstom, Philippe Delleur kwenye hotel ya Intercontinental jijini Paris Ufaransa , Julai 8, 2026. Mheshimiwa Mwigulu alikwenda Ufaransa kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Kilele cha Maadhimisho ya tano ya Siku ya Kiswahili Duniani . Kampuni hiyo inakusudia kuwekeza kwenye ujenzi wa reli ya kusafirisha abiria jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Alstom, Jean Francois kuhusu michoro iliyopendekezwa ya ujenzi wa reli ya kusafirisha abiria jijini Dar es salaam katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye hoteli ya Intercontinental jijini Paris, Julai 8, 2026. Kampuni hiyo inakusudia kuwekeza kwenye ujenzi wa reli ya kusafirisha abiria jijini Dar es salaam. Kulia ni Julie Morel wa kampuni hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
PMO 0829 Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na Makamu wa Rais Mwandamizi wa Kampuni ya Alstom, Philippe Delleur (kulia) kwenye hotel ya Intercontinental jijini Paris Ufaransa , Julai 8, 2026. Mheshimiwa Mwigulu alikwenda Ufaransa kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Kilele cha Maadhimisho ya tano ya Siku ya Kiswahili Duniani . Kampuni hiyo inakusudia kuwekeza kwenye ujenzi wa reli ya kusafirisha abiria jijini Dar es salaam. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Jean Francois, Julie Morel na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Saidi Othman Yakub.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Yaonesha nia ya kushirikiana na Serikali katika usafiri ya Mijini.
Dkt. Mwigulu awahakikishia mazingira bora ya uwekezaji
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekutana na Makamu wa Rais wa Kampuni ya ALSTOM ya nchini Ufaransa, Philippe Deller ambapo wamejadiliana kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya miundombinu ya usafiri nchini Tanzania.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mwigulu Nchemba aliikaribisha ALSTOM kuwekeza nchini, akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kutekeleza mageuzi yanayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara, usafiri na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa Upande wake Bw. Phillepe alieleza nia ya kampuni hiyo kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya usafiri wa mijini.
Kampuni hiyo imeonesha utayari wa kuwekeza katika ujenzi wa mifumo ya usafiri wa haraka na miundombinu ya kisasa yenye lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, huku ikitazama pia fursa za utekelezaji wa miradi kama hiyo katika majiji ya Mwanza, Mbeya na Arusha.
Miradi hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri wa mijini, kupunguza muda wa safari, kuimarisha shughuli za biashara na uwekezaji, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa.
Mazungumzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha ushirikiano na kampuni kubwa za kimataifa ili kuleta teknolojia, utaalamu na mitaji inayochochea maendeleo ya miundombinu na uchumi wa Taifa.
Kampuni ya ALSTOM, ina uzoefu mkubwa katika kubuni, kujenga na kuendesha mifumo ya kisasa ya usafiri wa umma ikiwemo reli za kisasa, treni za mwendo kasi, metro, tram na teknolojia za usimamizi wa usafiri.
