Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesema mafanikio ya Hati Fungani ya iTrust Finance Limited (iTrust Bond) yameweka rekodi mpya katika masoko ya mitaji nchini baada ya kuvutia maombi ya uwekezaji yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 114, sawa na mafanikio ya asilimia 760.78 ya lengo lililowekwa.
Akizungumza katika hafla ya kuorodheshwa kwa Hati Fungani hiyo kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) iliyofanyika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam Julai 8, 2026, Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, CPA Nicodemus D. Mkama, alisema mafanikio hayo yanaonyesha kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika masoko ya mitaji nchini.
“Hii ni historia mpya kwa soko letu la mitaji. iTrust Bond imevunja rekodi ya hati fungani zote zilizowahi kutolewa nchini na ni ushahidi kuwa wawekezaji wanaendelea kuamini fursa zinazopatikana kupitia masoko ya mitaji,” alisema Mkama.
Alisema kuorodheshwa kwa hati fungani hiyo kunaongeza kina cha soko la mitaji, kunapanua fursa za uwekezaji na kuwezesha kampuni binafsi kupata mtaji wa muda mrefu kwa ajili ya kukuza biashara na kuchangia maendeleo ya uchumi.
Mkama alieleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na maboresho yaliyofanywa na CMSA, ikiwemo kupunguza kiwango cha chini cha uwekezaji hadi Shilingi 500,000, kuruhusu malipo ya riba kila baada ya miezi mitatu na matumizi ya mifumo ya kidijitali ambayo imeongeza ushiriki wa wawekezaji.
Aidha, aliipongeza iTrust Finance kwa kutumia masoko ya mitaji kukuza biashara zake, akisema hatua hiyo inaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi.
Alizitaka kampuni na taasisi nyingine kutumia masoko ya mitaji kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo, huku akisisitiza kuwa CMSA itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuhamasisha wananchi kushiriki zaidi katika masoko ya mitaji.

